kupiga vita mila potofu ambazo ni chanzo ukatili wa kijinsia

Katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, Wakazi wa Kata ya Luanga Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya wametakiwa kupiga vita mila potofu ambazo ni chanzo ukatili wa kijinsia.

Wito huo umetolewa hii leo Novemba 28, 2023 na Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Mbeya Mkaguzi wa Polisi, Lovenes Mtemi katika kampeni ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.

Amesema, “acheni kukumbatia mila potofu, ukeketaji na ngoma za asili ambazo husababisha vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa kwa watoto na wanawake.”

Naye Afisa maendeleo ya jamii Wilaya ya Mbarali, Neema Swila amekemea makundi ya kijamii ambayo yanashindwa kutimiza wajibu wao katika suala nzima la malezi ya mtoto.

“Timizeni wajibu wenu katika malezi ya watoto, acheni kupeleka watoto kwa bibi na babu, jukumu la malezi ni la wazazi, baba na mama” Alisema Bi.Neema Swila.

Nao wazee wa kimila, wazee mashuhuri na viongozi wa dini waliohudhuria kampeni hiyo, wamekemea mila potofu kama vile ngoma za chakulaga kwa kusema ni chanzo cha vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa kwa mabinti na wanawake.

Elimu hiyo imetolewa kwa ushirikiano wa Jeshi la Polisi Dawati la Jinsia na Watoto, Ofisi ya Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Mbarali na Shirika lisilo kuwa la Kiserikali la TUMAINI.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!