Dalili za Ugonjwa unaojulikana kama PCOS(Polycystic Ovarian Syndrome)

Dalili za Ugonjwa unaojulikana kama PCOS(Polycystic Ovarian Syndrome)

Kirefu cha neno PCOS ni Polycystic Ovarian Syndrome. Syndrome maana yake ni tatizo lenye mkusanyiko wa dalili zaidi ya moja. Hivyo PCOS ni ugonjwa wenye dalili mbali mbali mwilini unao jitokeza kwa wanawake walio kwenye umri wa kuzaa.

Nini chanzo cha PCOS?

Mpaka hivi sasa chanzo cha ugonjwa huu haujajulikana, ila inasemekana tatizo hili linaweza kujitokeza kutokana na mambo mbali mbali. Mfano unaweza ukarithi au ukaupata kutokana na mabadiliko ya homoni mwilini na vilevile unaweza ukapata kutokana na aina ya maisha na mazingira unayoishi.

Dalili za mtu mwenye PCOS:

  • Kutokuwa na mpangilio wa siku za hedhi:

Mwanamke anaweza akawa haoni siku zake kwa miezi kadhaa na hii hujitokeza kwa sababu ya ukosekanaji wa upevukaji wa mayai. Kutokana na hali hii, mwanamke anakuwa anatengeneza homoni za estrogen kwa mda mrefu zinazo sababisha ukuta wa ndani wa mji wa mimba kuwa mnene zaidi ya kawaida na kusababisha kupata damu nyingi na maumivu makali kuliko kawaida wakati wa hedhi.

  • Kuota nywele nyingi kuliko kawaida:

Mwanamke mwenye tatizo hili anapata kuotwa na nywele nyingi kuliko kawaida. Maeneo yanayoathirika ni pamoja na mikononi, miguuni, kifuani, tumboni na usoni. Dalili hizi zinajitokeza kutokana na uzalishwaji mkubwa wa homoni za kiume (androgens).

  • Chunusi:

Tatizo hili linaweza kuleta uotaji wa chunusi ulio kithiri katika maeneo ya uso, kifua na mgongoni. Chunusi hujitokeza kwa sababu ya uzalishwaji mkubwa wa mafuta mazito kwenye matundu ya nywele ya Ngozi. Mafuta haya yanapoziba vitundu vya vinyoleo vinaishia kutengeneza chunusi na chanzo cha mafuta haya ni ongezeko na homoni za kiume mwilini.

  • Uvimbe kwenye mifuko ya mayai:

Manawake wenye PCOS huwa wanapata viuvimbe vingi vilivyojaa maji na vidogo vidogo kwenye mifuko ya mayai. Hii inatokana na mayai kushindwa kupevuka na kuishia kutengeneza viuvimbe maji kwenye mifuko hiyo.

  • Ugumba (infertility):

Ugumba ni hali ambayo mwanamke anashindwa kupata ujauzito. Kwa wale wenye PCOS sababu ya kushindwa kupata ujauzito ni kutokana na mayai kushindwa kupevuka.

  • Uzito ulio kithiri (obesity):

Uongezekaji wa uzito ulio kithiri ni moja kati ya dalili za PCOS. Mwanamke mwenye tatizo hili miili yao huwa ina changamoto katika matumizi ya homoni iitwayo insulini. Utengenezwaji mkubwa wa homoni ya insulin inasababisha matuta kuifadhiwa kwa wingi mwilini na ndio chanzo cha kuongezeka uzito.

Nini ufanye ukiwa na dalili hizi?

  • Unapokuwa na hizi dalili tunashauri uonane na daktari ili ufanyiwe uchunguzi wa kina na kuanzishiwa matibabu.
  • kuwa mvumilivu wakati wa tiba kwani matibabu juu ya tatizo hili ni ya mda mrefu.
  • Ni vyema kutambua kwamba matibabu ya hili tatizo yanatofauniana baina ya mtu na mtu.

Via:Dr.Kitange

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!