Kushambuliwa kwa hospitali na kukatwa kwa mawasiliano ni pigo kubwa kwa mfumo wa afya na raia Gaza: UN

Kushambuliwa kwa hospitali na kukatwa kwa mawasiliano ni pigo kubwa kwa mfumo wa afya na raia Gaza: UN

Watu wanaokimbia mapigano huko Gaza wanaendelea kutafuta maeneo salama ya kujihifadhi katika eneo hilo.

Hali ya kibinadamu inazidi kuwa mbayá katika Ukanda wa Gaza Mashariki ya Kati, huku hospitali zilizosalia zikiendelea kushambuliwa na kukatili maisha ya watu na kufungwa kwa mawasiliano ya simu na mtandao wa intanet vikizidisha adha yameonya leo mashirika ya Umoja wa Mataifa.

Hali si hali Gaza maisha ya watu yanaendelea kupotea kila siku kwanza kutokana na mashambulizi lakini pia kwa kukosa huduma muhimu za afya kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus ambaye kupitia ukurasa wake wa X hii leo amesisitiza kwamba “Mashambulizi dhidi ya hospitali , wahudumu wa afya na wagonjwa lazima yakome na usitishwaji mapigano ufanyike sasa”

Dkt. Tedros pia amelaani vikali uharibifu mkubwa uliofanyika katika hospitali ya Kamal Adwan Kaskazini mwa Gaza baada ya kuvamiwa na vikosi vya Israel mwishoni mwa wiki  ambapo wagonjwa wanane wameuawa akiwemo mtoto wa miaka 9.

Ameongeza kuwa wiki iliyopita vikosi vya Israel kwa siku nne viliivamia hospitali hiyo na kuipekua ndani nje huku kukiwa na taarifa za wahudumu wengi wa afya kushikiliwa.

Dkt. Tedros ameonya kwamba “Mfumo wa afya wa Gaza ambao tayari ulikuwa taaban sasa kupoteza hospitali nyingine hata kama inafanya kazi kwa kiasi kidogo ni pigo kubwa kwa watu wa Gaza.”

Kivuko cha Shalom Karem (kutoka Maktaba)

Mahema ya watu waliofurushwa makwao yamesambaratishwa

Mkuu huyo wa WHO amesema wagonjwa wengi huko Kamal Adwan walilazimika kujiondoa “katika hatari kubwa kwa afya na usalama wao” huku magari ya kubeba wagonjwa yakishindwa kufika kituoni.

Ofisi yaUmoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharira OCHA imesema katika tarifa yake kwamba siku ya Jumamosi vikosi vya Israeli viliondoka hospitalini na kulingana na ripoti za vyombo vya habari “buldoza la jeshi la Israeli lilisambaratisha mahema ya wakimbizi wa ndani nje ya hospitali, na kuua na kujeruhi idadi ambayo haijathibitishwa watu”.

Tedros alisema kwenye mtandao wake wa X kwamba WHO “inajali sana ustawi wa watu hao waliolazimika kukimbia makwao.”.

Kwa mujibu wa OCHA wizara ya afya ya Palestina mjini Ramallah imetaka uchunguzi ufanyike kuhusu tukio hilo.

OCHA pia ilinukuu jeshi la Israel likisema kuwa limewashikilia watu 90 kama sehemu ya operesheni hiyo na “limepata silaha na risasi ndani ya hospitali”.

Kukatika kwa mawasiliano

Kutokana na kukatika kwa mawasiliano ya simu na mtandao wa internet huko Gaza ambao ulianza Alhamisi iliyopita na kuendelea hadi mwishoni mwa wiki, OCHA imesisitiza katika tarifa yake ya hivi karibuni kwamba kuhusu hali ya kibinadamu katika Ukanda huo tarifa ni finyu  kuanzia saa 24 zilizopita.

Huku shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limesema “Gaza nzima sasa hakuna taarifa mpya zinazopatikana za vifo na majeruhi.”

Limeongeza kuwa katika Ukingo wa Magharibi tangu kuanza kwa mzozo huu mpya Wapalestina 268 wameuawa na vikosi vya Israel wakiwemo watoto 70 ikiwa ni idadi kubwa Zaidi ya vifo vya Wapalestina kwa mwaka.

Shirika hilo limeonya kwamba kuendelesha kwa mashambulizi kwenye Ukanda wa Gaza kunasababisha ugumu mkubwa wa kuafikia wenye uhitaji na hivyo kuwafanya watu waendelee kuwa katikati ya vita, kuzingirwa na kukosa mahitaji.

OCHA imesema nako Gaza mamlaka ya afya ya Gaza haijasasisha idadi yao ya majeruhi tangu kuanza kwa kukatika kwa umeme, ambayo wakati huo ilikuwa imefikia vifo 18,787 na zaidi ya watu 50,000 kujeruhiwa tangu 7 Oktoba.

Kuendelea kwa mashambulizi ni hatari kubwa

Ofisi hiyo imeripoti kuendelea kwa “mashambulizi mazito ya Israel katika Ukanda huo mwishoni mwa juma hasa huko Khan Younis kusini mwa Gaza na katika maeneo kadhaa ya mji wa Gaza kaskazini.”

Mapigano makali yalizuka kati ya wanajeshi wa Israel na makundi yenye silaha ya Palestina huko Khan Younis na Rafah, pamoja na kuendelea kurusha makombora na makundi ya wapalestina yenye silaha nchini Israel, OCHA imesema.

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF ambalo linasema ushitishwaji haraka wa mapigano wa muda mrefu kwa minajili ya kibinadamu ni lazima kwani sasa eneo zima la Gaza ambako Watoto walikuwa wakicheza na Kwenda shuleni kufurahia utoto wao limegeuka kifusi na kuwaacha njiapanda watoto hao.

Kivuko cha mpaka cha Kerem Shalom. (Maktaba)

Kivuko cha pili kimefunguliwa kwa msaada

Hali ya kibinaadamu katika eneo hilo bado ni mbaya kwani idadi kubwa ya watu wamelazimika kuyahama makazi yao, wamesongamana katika eneo dogo kusini, wakikabiliwa na hali mbaya ya usafi na kukosa chakula na maji.

Umoja wa Mataifa unasema matumaini ya kuongezwa kwa misaada yameongezeka kutokana na tangazo la Ijumaa la kufunguliwa kwa kivuko cha mpaka cha Kerem Shalom kati ya Israel na Gaza, ambacho kulikaribishwa na jumuiya ya misaada.

Kivuko hicho kinaripotiwa kufunguliwa Jumapili kwa mara ya kwanza tangu tarehe 7 Oktoba.

Hadi wakati huu ni kivuko cha mpaka cha Rafah kusini pekee ndicho kilikuwa kimefunguliwa tangu usafirishaji wa misaada urejeshwe tarehe 21 Oktoba.

“Utekelezaji wa haraka wa makubaliano haya utaongeza mtiririko wa misaada,” amesema mkuu wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya dharura Martin Griffiths, na kuongeza kuwa “lakini kile ambacho watu wa Gaza wanahitaji zaidi ni kumalizika kwa vita hivi”.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!