WANANCHI ZINGATIENI KANUNI ZA AFYA KUJIKINGA NA MAGONJWA YA MFUMO WA HEWA
Mganga mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu amewata wananchi kuzingatia kanuni za afya kwa kuzingatia usafi na kupata chanjo ya UVIKO 19 kwa ukamilifu ili kujikinga na magonjwa ya njia ya hewa ikiwemo mafua, kikohozi, kupumua kwa shida, kuwashwa koo, homa na kuumwa kichwa.
Prof. Nagu ameyasema hayo kufuatia tetesi za kuongezeka kwa magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa ambapo amesema magonjwa ya mfumo wa hewa yapo muda wote Nchini huku akibainisha kwamba kumekuwepo na vipindi vya kuongezeka na kupungua kwa visa hivi kwa nyakati tofauti katika mwaka.
Aidha Prof. Nagu amesema Wizara imekuwa ikifanya ufuatiliaji wa taarifa za magonjwa ya mlipuko ikiwa ni pamoja na tetesi za kuwepo kwa magonjwa hayo ndani na nje ya Nchi ambapo kuanzia November, 2023 kumekuwa na tetesi juu ya ongezeko la visa vya magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa sehemu mbalimbali duniani na ndani ya nchi hususan Dar es salaam ambapo amesema Uviko 19 umeendelea kuwepo kwa kiwango cha chini kama magonjwa mengine ya mfumo wa njia ya hewa ukiongezeka na kupungua kwa nyakati tofauti za majira ya mwaka.
Prof. Nagu amesema virusi vya Influenza vilivyobainika nchini havina madhara makubwa ndio maana unaitwa ugonjwa wa majira (Seasonal Influenza) lakini hata hivyo takwimu za ufualitiliaji (surveilance) za Wizara zinaonesha ongezeko la maambukizi ya Uviko 19 kutoka 37 mwezi October 2023 hadi maambukizi 65 mwezi December 2023”
“Aidha, ongezeko hili ni sambamba na ongezeko la maambukizi ya mafua yanayotokana na influenza kutoka maambukizi 34 hadi 49 katika kipindi hicho hicho”. Amesema Prof Nagu.
Wizara inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa na inaelekeza Wataalamu katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya kuendelea kufanya utambuzi kwa njia ya vipimo vya maabara na kutoa matibabu stahiki, huku ikiwashauri Wananchi kuwahi kwenye Vituo vya kutolea huduma mara wapatapo dalili za magoniwa ya mfumo wa njia ya hewa zikiwemo mafua, kikohozi, kuwashwa koo, kupumua kwa shida, homa na kuumwa kichwa.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!