Magonjwa yasiyo ya kuambukiza yatajwa kusababisha asilimia 36% ya Vifo

Magonjwa yasiyo ya kuambukiza yatajwa kusababisha asilimia 36% ya Vifo.

Asilimia 36 ya vifo nchini vinasababishwa na magonjwa  yasiyo ya kuambukiza, huku gharama za dawa zake zikiwa juu.

Hayo yamebainishwa  jana Desemba 14,2023 katika semina ya Waandishi wa Habari iliyoandaliwa na Chama Cha Wanasheria Wanawake Nchini (TAWLA), juu ya uchambuzi wa sheria ya mtindo wa maisha na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ili kusaidia jamii kupitia sheria.

Akizungumza katika semina hiyo Dk. Fredrick  Mashil kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS)  amesema  magonjwa hayo yanaweza kuzuilika  kwa kuzingatia lishe bora na mtindo mzuri wa maisha.

“Vitu vikubwa viwili vinasababisha mangonjwa yasiyo ya kuambukiza ni ‘diet’, kufanya mazoezi  kupitiliza na mtindo  wa maisha,” amesema Dk. Mashil.

Amesema  hakuna sheria na sera yoyote ambayo inazuia  kula vyakula ambavyo vinaathiri afya ya walaji.

“Nimefanya utafiti wa mafuta ya kula yanayotumiwa na watu wengi  yanayotokana na mboga mboga ni mazuri kiafya, ila  mafuta  ya kula yatokanayo na wanyama sio mazuri   kiafya, nashauri watu watumie mafuta ya kula yanatokana na  mboga mboga,” ameeleza.

Mwenyekiti wa Chama cha Vijana wenye Kisukari Tanzania (TDYA),George Kwayu.

Ameongeza kuwa zaidi  ya vifo  25000 vinaweza kupungua kwa kuondoa  bidhaa zinazoathiri afya ya walaji.

Akizungumzia kuhusu  kufanya  mazoezi, Dk. Waziri Ndonde  amesema jamii inatakiwa kujiepusha na tabia bwete na kuhakikisha wanafanya shughuli tofauti kila baada ya dakika 60 kama vile kusimama,kutembea,kukimbia au jambo lolote la kughulisha mwili.

“Amebainisha kuwa katika kanuni bora za afya ya mwili na akili watoto na vijana kati ya miaka 5-17 wanatakiwa kutumia dakika 60 katika michezo na mambo ya kushughulisha mwili kila siku.

“Kwa upande wa watu wazima kati ya miaka 18-64 na pamoja na watu wenye magonjwa sugu wanashauriwa kutumia dakika 150 kwa wiki ndani ya siku tano wafanye mazoezi ya uzito wa kati na siku mbili wanatakiwa kufanya mazoezi ya misuri ndani ya dakika 30,” amesema Dk. Ndonde.

Amesema ili kujenga mwili ni lazima kufanya kazi za kuushughulisha kama vile kutembea,kukimbia,kufanyakazi za nyumbani,kutumia baiskeli,kushiriki kwenye michezo mbalimbali.

“Kama unafanya mazoezi peke yake na hivi vingine huvifanyi, ndio utasikia mtu anasema mimi naenda gym lakini kila siku lakini sipungui,” amesema.

Dk.Ndonde amesema watu wenye ulemavu wao wanapaswa kufanya mazoezi kwa dakika 300 kwa wiki.

Pia amesisitiza kuwa wanawake wajawazito na waliojifungua wanapaswa kufanya mazoezi kwa dakika 150 kwa wiki.

“Tafiti zinaonyesha kujifungua na kunyonyesha sio sababu ya kunenepa, watu wengi wanakula kupitiliza na kuacha mazoezi pindi wanapojifungua,”amesema.

Ameongeza kuwa kufanya mazoezi kunaufanya ubongo wako unafanyakazi vizuri pia inaongeza uwezo wa moyo kufanya kazi vizuri.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Vijana wenye Kisukari Tanzania ( TDYA), George Kwayu amesema  mtu yeyote anaweza kuwa na ugonjwa  wa kisukari, hivyo  ni jambo  la kujikubali.

“Japo kuna changamoto za mara kwa mara ikiwemo jamii kuto wakubali vijana  wanaokuwa na ugonjwa wa kisukari,vijana  wengi wamepoteza kazi kwa sababu hakuna uelewa kwa watu na jinsi gani ya kuishi nao,”amesema Kwayu.

Ameeleza  kuwa matibabu  ya ugonjwa wa kisukari  ni gharama  kubwa, ndani  ya mwezi  Desemba  amepoteza vijana saba na serikali  itambue kwenye magonjwa  yasiyo ya kuambukiza  kuna changamoto gani

Aidha Kwayu amewashauri wagonjwa  wa kisukari  kwamba matibabu  ya sukari  yanapatikana hospitali  na kuna watalaamu wazuri.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!