TMDA yataja mikoa vinara wizi wa dawa za Serikali

Mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Simiyu imetajwa kuwa vinara wa uchepushaji wa dawa za Serikali kwa mujibu wa Mamlaka ya Dawa, Vifaa Tiba na Vitendanishi Tanzania (TMDA).

Operesheni iliyofanyika imekamata dawa kadhaa zikiwemo dawa zenye asili ya kulevya na zile za nusu kaputi zilizokutwa kwenye maduka ya dawa ambazo haziruhusiwi kuuzwa nje ya hospitali.

Hayo yamesemwa leo Jumatano, Desemba 20, 2023 na Mkurugenzi Mkuu, Adam Fimbo wakati akitoa matokeo ya operesheni maalum ya kukamata dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya Serikali, bandia, duni, zisizo na usajili na dawa za kulevya.

“Vifaa tiba vya Serikali vinavyokadiriwa kuwa na thamani ya Sh11,297,500 milioni vilikamatwa katika vituo na maduka binafsi.

“Baadhi ya vifaa tiba hivyo ni pamoja ni IV Cannula G21, G20, G22, vifaa vya kupima Malaria na Virusi vya Ukimwi, Hemocue Glocose201, Microcuvettes na Hemocue Hb2021 ambavyo vilikamatwa Kanda ya Mashariki na Kanda ya Kati,” amesema Fimbo.

Amesema Jumla ya bidhaa zenye thamani ya Sh172 milioni zimekamatwa katika operesheni hiyo.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!