Ticker

6/recent/ticker-posts

Wagonjwa wa Upasuaji wanangoja kufa kaskazini mwa Gaza:WHO



Wagonjwa wa Upasuaji wanangoja kufa kaskazini mwa Gaza:WHO.

Mvulana mwenye umri wa miaka 3, ambaye nyumba yake ilishambuliwa kwa bomu, anapata nafuu katika hospitali ya Nasser baada ya kukatwa sehemu ya mguu wake wa kulia.

Hakuna hospitali zinazofanya kazi kaskazini mwa Gaza na wagonjwa waliojeruhiwa ambao wanahitaji upasuaji na hawawezi kuhamishwa “wanangoja kufa”, limesema jana shirika la afya Duniani WHO, katika ombi lake la kusitishwa kwa mapigano ili kuruhusu msaada zaidi katika eneo hilo lililosambaratika.

Tathmini hiyo ya hivi karibuni kabisa kutoka kwa WHO imekuja baada ya timu za Umoja wa Mataifa kufika hospitali ya Al Ahli Arab na hospitali ya Al Shifa juzi Jumatano, wakati kukiwa na ripoti za kuimarisha operesheni za ardhini za vikosi vya ulinzi vya Israel na kuendelea na mashambulizi ya anga katika Ukanda wa Gaza, ili kukabiliana na mashambulizi ya kigaidi ya Hamas ya tarehe 7 Oktoba kusini mwa Israel.

Mratibu wa timu za dharura za WHO, Sean Casey amesema “Wagonjwa walikuwa wakilia kwa maumivu, lakini pia walikuwa wakilia tuwape maji,” akielezea tukio katika hospitali ya Al Ahli Arab, ambapo wahudumu wa afya walikuwa wakijitahidi kukabiliana na hali huku kukiwa hakuna chakula, hakuna mafuta na hakuna maji.

Ameongeza kuwa “Hivi sasa inaonekana zaidi kama kituo cha wanaosubiri kifo badala ya hospitali. Lakini ni kituo cha wagonjwa mahututi kinachomaanisha kiwango cha huduma ambacho madaktari na wauguzi hawawezi kutoa. Ni jambo lisiloweza kuvumilika kuona mtu aliye na vidonda  vya majeraha katika miguu na mikono na wengine kwenye viungo vingi, bila maji ya kunywa na karibu hakuna hata drip zinazopatikana.”

Amesema “Kwa sasa, ni mahali ambapo watu wanangoja kufa watanusurika tu endapo tunaweza kuwahamisha hadi mahali salama ambapo wanaweza kupata huduma.”

Vifaa vya afya vinatayarishwa kwa usafirishaji hadi Gaza. (Maktaba)

Wito wa misaada wa Guterres

Akiangazia haja ya kukabiliana na mzozo wa kibinadamu unaozidi kuzorota huko Gaza, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres leo amesema kwamba “mapigano makali, ukosefu wa umeme, mafuta kidogo na kutatiza mawasiliano ya simu” vimezuia sana juhudi za Umoja wa Mataifa kutoa msaada wa kuokoa maisha kwa watu katika eneo hilo linalokaliwa.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kupitia ukurasa wake wa X kuwa “Hatua za kuruhusu operesheni kubwa za kibinadamu zinahitaji kuanzishwa tena mara moja,”

Kuongezeka kwa njaa

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa uliokwenda Gaza ambao umehusisha WHO, ofisi ya kuratibu misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, OCHA, Ofisi ya Huduma ya Umoja wa Mataifa inayohusika na uteguaji wa mabomu UNMAS na Idara ya Usalama ya Umoja wa Mataifa UNDSS ilihakikisha utoaji wa makasha saba ya dawa zinazohitajika haraka, maji ambayo ni tiba au drips na vifaa vya upasuaji na kutibu waliojeruhiwa, pamoja na vifaa vya kusaidia wanawake wanaojifungua.

Wamesema muhimu ni utoaji wa vifaa vya matibabu kaskazini ili kuleta afuaeni kwa wagonjwa, na kinachotia wasiwasi zaidi ni kuongezeka na tayari kuenea kwa uhaba wa chakula na maji.

“Tuko nyuma. Hakuna chakula cha kutosha, kila mtu ninayezungumza naye kila mahali ninapoenda Gaza ana njaa,” amesema  Bwana Casey akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva.

Ameongeza kuwa “Wakati ni sasa wa kunashughulikia nwatu wenye njaa sasa, watu wazima, watoto, njaa haivumiliki. Kila mahali tunapokwenda, watu wanatuomba chakula hata hospitalini, nilizunguka katika idara ya dharura, mtu aliye na jeraha la wazi la damu, waliovunjika viungo wote wanaomba chakula. Ikiwa hiyo sio kiashiria cha kukata tamaa, sijui ni nini.”

Kulingana na WHO ni vituo tisa tu kati ya 36 vya afya huko Gaza ambavyo vinafanya kazi kwa kiasi vingine vyote viko kusini.

“Hakuna vyumba vya upasuaji kaskazini mwaka Gaza  tena kwa sababu ya ukosefu wa mafuta, nishati, vifaa vya matibabu na wafanyikazi wa afya, wakiwemo madaktari wa upasuaji na wataalamu wengine,” amesema Dkt Richard Peeperkorn, Mwakilishi wa WHO na sasa pia ni kaimu mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa katika eneo lililokaliwa la Palestina, akizungumza kutoka Jerusalem.

Katika hospitali ya Al Ahli Arab takriban wafanyakazi 10 “wote madaktari wadogo na wauguzi wameendelea kutoa huduma ya kwanza ya msingi kwa wagonjwa 80 ambao sasa wamehifadhiwa katika kanisa ndani ya uwanja wa hospitali,” ameeeleza Dkt. Peeperkorn.

Ameendelea kusema kwamba “Baadhi yao wamejeruhiwa vibaya na wanasubiri kufanyiwa upasuaji kwa wiki mbili sasa au wamefanyiwa upasuaji lakini sasa wako hatarini kupata maambukizi baada ya upasuaji huo kutokana na kukosa dawa za kuua vijiuavijasumu na dawa nyinginezo.

Wagonjwa hawa wote hawawezi kutembea na wanahitaji kuhamishwa haraka, ili kupata fursa ya kuishi.

Wanawake wa Kipalestina wakiomboleza kifo cha mwanafamilia mmoja katika Hospitali ya Matibabu ya Al-Nasser huko Khan Younis, kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Mashambulizi ya mabomu na mapigano makali

Kwa mujibu wa taarifa mpya za ofisi ya OCHA kuhusu mgogoro huo, “mashambulizi makubwa ya mabomu ya Israel kutoka angani, ardhini na baharini, yaliendelea kote Gaza jana Jumatano.”

Mashambulizi makali zaidi ya makombora yaliripotiwa huko Beit Lahiya na maeneo mengi katika mji wa Gaza kaskazini, mashariki mwa Khan Younis ,kusini na maeneo ya mashariki na magharibi ya mji wa Rafah, pia Kusini mwa Gaza.

OCHA pia imeripoti “operesheni kali za ardhini” na kuendelea kwa mapigano kati ya vikosi vya Israeli na vikundi vyenye silaha vya Palestina kaskazini mwa Gaza, Mji wa Gaza, eneo la Kati, na Khan Younis, pamoja na kurusha makombora na vikundi vyenye silaha vya Palestina kuelekea Israeli.

Takwimu za hivi karibuni kutoka kwa mamlaka ya afya ya Gaza zilizoshirikiwa na OCHA Jumanne zilionyesha kuwa Wapalestina 19,667 wameuawa huko Gaza tangu 7 Oktoba, karibu asilimia 70 wanaaminika kuwa wanawake na watoto.

Zaidi ya watu 52,586 wamejeruhiwa, kulingana na chanzo kimoja, ambacho kiliripoti kwamba wengi zaidi walipotea, ambapo inawezekana walifukiwa chini ya vifusi.

Taarifa ya Umoja wa Mataifa pia imebainisha kuwa wanajeshi wawili wa Israel waliripotiwa kuuawa huko Gaza kati ya tarehe 19 na 20 Disemba.

“Tangu kuanza kwa operesheni za ardhini, wanajeshi 134 wameuawa huko Gaza, na wanajeshi 740 wamejeruhiwa, kulingana na jeshi la Israeli,” imesema OCHA.

Agizo jipya la kuhama watu

Taarifa hiyo pia imeashiria amri mpya ya kuondolewa watu mara moja iliyotolewa  Disemba 20 na jeshi la Israeli inayojumuisha karibu asilimia 20 ya maeneo kati na kusini mwa jiji la Khan Younis.

Eneo hilo liliwekwa alama kwenye ramani ya mtandaoni iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii.

Kabla ya ongezeko la machafuko Oktoba 7, eneo hilo lilikuwa makazi ya karibu watu 111,542, kulingana na OCHA, ambayo imebainisha kuwa pia ni pamoja na makazi 32 ya wakimbizi wa ndani wapatao 141,451 wengi wao wakiwa wameyakimbia makazi yao hapo awali kutoka kaskazini.



Post a Comment

0 Comments