Wamiliki wa hospitali binafsi watishia kugoma kutoa huduma

Wamiliki wa hospitali binafsi watishia kugoma kutoa huduma.

Wamiliki wa hospitali binafsi nchini wametishia kugomea kutibu wagonjwa wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), iwapo bei mpya zilizotangazwa na mfuko huo zitaanza kutumika Januari Mosi kama ilivyopangwa. Anaripoti Mwandishi Wetu….(endelea)

Kupitia taarifa yao kwa vyombo vya habari jana, wamiliki hao wamesema kitita hicho kilipitishwa na serikali bila kuwashirikisha na kitasababisha hospitali nyingi kufungwa kutokana na kupata hasara  iwapo kitaanza kutumika.

“Kwa miaka saba sasa tangu gharama mpya zitangazwe hazikuwahi kuboreshwa na ilikuwa matarajio yetu kwamba NHIF itatangaza ongezeko la gharama za  huduma na siyo kupunguza,” ilisema na kuongeza

“Kwa kuzingatia ukweli huu pamoja na mengine kama ucheleweshaji wa malipo kwa zaidi ya miezi minne, mfumuko wa bei, kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola kwa zaidi ya asilimia 20 ndani ya miaka saba APHFTA tumeona tutashindwa tutashindwa kuwahudumia wanachama wa NHIF kama bei hizi zitaanza kutumika rasmi,” ilisema

Ilitoa mfano kuwa kushuka kwa gharama za kumwona daktari, upasuaji na kuchuja damu (dialysis), kutawafanya washindwe kumudu gharama halisi za kuhudumia wagonjwa wanaotibiwa kwao.

Ilisema bei za mwisho ziliwsekwa tangu mwaka 2016 na tangu wakati huo hazijwahi kufanyiwa mapitio licha ya gharama za maisha kupanda sasa kushusha gharama ni sawa na kuzichimbia kaburi hospitali binafsi.

“Malipo yenyewe kwa watoa huduma yanaweza kukaa miezi hata sita hayajalipwa na wakati mwingine wanakataa baadhi ya madai ya malipo bila sababu za msingi sasa haya yote hayajataatuliwa wanakuja kushusha gharama si wanataka kutuua,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa yao ilisema kuwa NHIF iliwaambia wafunge mfumo wa online kwaaajili ya kuwasilisha madai yao ya huduma wanazotoa ili wawe wanalipwa ndani ya siku 14 baada ya kuwasilisha madai hayo lakini hali bado ni ile ile tangu wafunge.

“Tumefunga mfumo ambao umetugharimu shilingi milioni 80 lakini hizo siku 14 walizosema hawalipi na bado tunalazimika kusubiri miezi minne hadi sita, kama wanaona gharama za uendeshaji zimekuwa kubwa wapunguze matumizi yao yasiyo ya lazima lakini watibu watu,” ilisema

“Kwenye hili tunamuomba Rais Samia Suluhu Hassan atusaidie kwasababu kwa hiki kitita ni kama wanataka kuzifunga hospitali binafsi, Rais wetu siku zote amekuwa akisisitiza ushirikishwaji wa sekta binafsi kupitia PPP lakini hawa ni kama hawataki kuona tuna survive,” ilisema

Ilisema APHFTA iliwasilisha mapendekezo ya namna ya kuboresha uhai wa mfuko ikiwemo kuitaka NHIF ipitie upya mapendekezo ya kibiashara kwa bidhaa zake vikiwemo vifurushi vya WEKEZA, TIMIZA, NAJALI na vinginevyo.

Ilisema walipendekeza NHIF itumie mfumo wa ukusanyaji madeni wenye ufanisi  zaidi na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesababu za Serikali (CAG) inamaelezo ya kiasi kikubwa cha fedha ambacho hakikusanywi na NHIF kwa taasisi nyingi.

“Kabla ya kutafuta suluhisho la nje NHIF inapaswa kuonyesha msimamo wa kupunguza gharama za uendeshaji ndani ya mfuko na tukumbuke kwamba vituo vya afya, hospitali na NHIF wanategemeana kwaajili ya kuishi na kuwa endelevu hivyo hatupaswi kudhoofishana,” ilisema

Ilisema kikao cha APHFTA kilikaa na kubaini kuwa baada ya ukaguzi wa madai ya Septemba, Oktoba na Novemba 2023 hospitali zote binafsi kuanzia ngazi ya Dispensari mpaka hospitali za rufaa zingepata hasara asilimia 25 kwa wastani.

“Na hii ni bila kuzingatia makato ya kila mwezi ukizingatia makato hayo yenye wastani wa asilimia 10 ambayo makato yenyewe yamejaa sintofahamu na utata mwingi yanafanya jumla ya hasara kufikia asilimia 35 kwa hospitali binafsi,” ilisema

Wakati huo huo, wakati wakati APHFTA inadai kutoshirikishwa katika mchakato wa kushusha gharama, NHIF wamesema waliwashirikisha katika hatua zote.

Kwenye barua yake kwa hospitali mbalimbali za Mkoa wa Dar es Salaam,  Meneja wa NHIF Mkoa wa Kinondoni, Dk. Christopher Lazeck alisema mwaka 2018 NHIF ilianza mchakato wa kuboresha kitita chake baada ya serikali kutoa mwongozo wa matibabu kwa lengo la kuwianisha  huduma za kitita cha mafao, mwongozo huo na bei ya soko.

Alisema kupitia barua yenye kumbukumbu namba EA.35/269/01-A/32 kuhusu dhamira ya mfuko ya kuanza kutumika kwa kitita cha mafao kwa lengo la kupata maoni, NHIF ilikutana na wadau na kupata maoni mbalimbali kwaajili ya maboresho zaidi.

“Lengo la maboresho ya yaliyofanyika ni pamoja na kuhuisha kitita cha mafao  na miongozo ya tiba nchini, kuweka usawa wa ada ya kumwona daktari bingwa kulingana na taaluma na ikama, kuboresha bei za huduma kulingana na hali halisi ya soko,” alisema

Alisema maboresho yalilenga kuongeza motisha kwa watoa huduma vikiwemo vituo vya ngazi ya Mkoa, Wilaya na vituo vya afya na Zahanati na kuwezesha huduma za kibingwa kupatikana karibu na Wananchi.

Chanzo: tanzaniaweb

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!