Aeleza alivyosaidiwa na Lowassa kupata matibabu ya ngozi KCMC
Aeleza alivyosaidiwa na Lowassa kupata matibabu ya ngozi KCMC
Asterina Banzi, aliyesaidiwa na Waziri Mkuu mstaafu, hayati Edward Lowassa kupata matibabu ya ngozi katika Hospitali ya KCMC
Asterina Banzi, mwenye ulemavu wa ngozi, ametoa ushuhuda wa msaada wa matibabu ya ngozi alioupata kwa Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa.
Ugumu wa kukutana na mwanasiasa aliyewahi kushika nafasi za juu za uongozi na ukamweleza shida zako, haukuwepo kwa Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa.
Hilo linathibitishwa na Asterina Banzi, mwenye ualbino anayeeleza alivyokutana na mwanasiasa huyo na kupatiwa msaada wa gharama za matibabu ya ugonjwa wa ngozi uliomsumbua kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa Asterina, mara yake ya kwanza kukutana na Lowassa ilikuwa mwaka 2015, katika kikao cha mwanasiasa huyo na watu wa makundi maalumu jijini Dar es Salaam.
Mwanadada huyo ameiambia Mwananchi Digital leo Jumanne, Februari 13, 2024 kuwa walipokutana na Lowassa katika kikao hicho aliomba namba zake za simu na alipewa na baadaye alimwandikia ujumbe mfupi wa kumweleza tatizo lake na siku chache baadaye alitafutwa na Lowassa kwa ajili ya kukutana kwa mazungumzo ya kina.
“Alinitaka tukutane, nilipofika eneo alilotaka tukutane akanambia nimweleze kuhusu tatizo langu. Nilimweleza, akanipa pole na kuniambia kwa sababu ya umri aliokuwa nao wakati huo asingeweza kunisaidia yeye binafsi, lakini atanipeleka kwa mtu atakayenisaidia,” amesema.
Amesema Lowassa alimpeleka kwa mtu huyo na hatimaye alipata msaada wa matibabu katika Hospitali ya KCMC na hadi sasa tatizo hilo limeisha.
“Ni mtu ambaye akishindwa kukusaidia yeye, anakupa namna anayoona utaupata msaada na nilifanikiwa hadi sasa nimepona,” amesema Asterina.
Asterina amesema tukio hilo litabaki kama kumbukumbu yake kwa Lowassa na kwamba hatamsahau mwanasiasa huyo.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!