Ticker

6/recent/ticker-posts

Kifo cha Dk Msabaha:Familia yaeleza alisumbuliwa na tatizo la nyonga, ugonjwa wa moyo muda mrefu



Kifo cha Dk Msabaha:Familia yaeleza alisumbuliwa na tatizo la nyonga, ugonjwa wa moyo muda mrefu.

Kusumbuliwa na tatizo la nyonga na ugonjwa wa moyo kwa muda mrefu ni mambo yanayotajwa kusabisha kifo cha aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Dk Ibrahim Msabaha (72).

Dk Msabaha aliyejiuzulu nafasi hiyo mwaka 2008 kutokana na sakata la Richimond, amefariki dunia jana Jumanne, Februari 13, 2024 wakati akiwa njiani kutoka nyumbani kwake, Masaki kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Jijini Dar es Salaam kupatiwa matibabu.

Akizungumza na Mwananchi Digital, msemaji wa familia hiyo, Abubakar Msabaha amesema changamoto hiyo ilikuwa ikimsumbua kwa muda mrefu na ilikuwa kawaida kupelekwa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kufanyiwa vipimo vya uangalizi mara kwa mara.

“Mzee wetu alikuwa anasumbuliwa na nyonga pamoja na ugonjwa wa moyo kwa muda mrefu sasa na daima tulikuwa tunamleta Taasisi ya Moyo kupatiwa matibabu na hadi jana alikuwa kawaida,” amesema Abubakar.

Amesema hata mwezi uliopita alilazwa katika taasisi hiyo mara mbili kwa matatizo hayo hadi hali yake ilipokuwa sawa aliruhusiwa kurudi nyumbani.

“Afya yake ilivyokuwa ikibadilika tulikuwa tunamkimbiza hospitalini hapo kupatiwa matubabu,” amesema.

Amesema mipango na ratiba za mazishi ya Dk Msabaha ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki na mbunge wa Kibaha, inaendelea na Leo, Februari 14, 2024 saa tisa alasiri wanatarajia kumzika katika kijiji cha Soga kilichopo Kongwe, Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani.



Post a Comment

0 Comments