Mtindo mbaya wa Maisha janga kwa Magonjwa yasioambukiza.
Jamii imetakiwa kuzingatia mtindo bora wa maisha na kufuata ulaji sahihi kama wanavyoshauriwa na wataalam wa afya ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa ya figo.
Hayo yamesema jana na Dkt.Gunini Kamba, akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam ambaye alikua mgeni rasmi katika hafla fupi ya kukabidhi tuzo na medali kwa baadhi ya watumishi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na taasisi nyingine zilizotolewa na Taasisi ya Profesa Jay ikiwa ni kutambua mchango wao katika kutoa huduma za afya.
Dr. Kamba amesema magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa ya figo yanazidi kuongezeka na gharama za matibabu kwa magonjwa hayo ni kubwa na si kila mwananchi anayeweza kumudu gharama hizo hivyo ni vyema jamii ikatambua hilo ili iweze kujikingwa kwa kuwa king ani bora kuliko tiba.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Ellen Senkoro ameipongeza Taasisi ya Professor Jay kwa kutambua mchango mkubwa unaofanywa na Hospitali ya Muhimbili na kuwapongeza baadhi ya watumishi ambao wamechaguliwa kupata tuzo hizo na kusema kuwa Muhimbili itaendelea kutoa mchango kwa tasisi hiyo ili indelee kutoa hamasa kwa jamii kuhusu afya.
Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi amesema kuwa kwa siku MNH-Upanga inatoa huduma ya kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo 120 hadi 130 ambapo asilimia 90 ya magonjwa wa hayo yanasababishwa ya shinikizo la juu la damu pamoja na kisukari ambapo chanzo chake nikutozingatia lishe sahihi hivyo ni vyema watu wakazingatia swala la lishe bora.
Awali akizungumza baada ya kukabidhi tuzo hizo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Professor Jay Florian Rutabingwa amesema taasisi hiyo itaendelea kutoa elimu ya afya kwa jamii ili kusaidia jamii kujikinga na magonjwa hayo ambayo yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!