TMA:vipindi vya mvua kubwa vinaweza kujitokeza
Kaimu Mkurugenzi wa TMA, Dk Ladislaus Chang’a (kushoto) akitoa taarifa ya uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa msimu wa mvua za Masika katika kipindi cha Machi hadi Mei, 2024.
Kwa mujibu wa TMA mvua hizo zinatarajiwa kuisha mwishoni mwa Mei
Dar es Salaam. Mamlaka za maafa nchini zimeshauriwa kuendelea kuratibu utekelezaji wa mipango itakayosaidia kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua za masika.
Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) imetoa tahadhari ikieleza vipindi vya mvua kubwa vinaweza kujitokeza na kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi, hivyo kusababisha uharibifu wa miundombinu, mazingira, upotevu wa mali na maisha.
Kaimu Mkurugenzi wa TMA, Dk Ladislaus Chang’a amesema hayo leo Februari 22, 2024 alipotoa taarifa ya uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa msimu wa mvua za Masika katika kipindi cha Machi hadi Mei, 2024.
TMA imesema kutakuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani kwa msimu wa masika, 2024 katika maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka. Ongezeko la mvua linatarajiwa Machi.
Dk Chang’a amesema mvua za masika zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya Februari katika maeneo mengi na zinatarajiwa kuisha wiki ya tatu na ya nne ya Mei, 2024 katika maeneo mengi.
Athari zinazotarajiwa
Amesema vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo.
Pia, kina cha maji katika mito na mabwawa kinatarajiwa kuongezeka, na magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza kutokana na uchafuzi wa maji.
Amesema athari za kisekta na ushauri uliotolewa umeandaliwa na TMA kwa kushirikiana na wataalamu wa sekta husika katika mkutano wa wadau wa hali ya hewa uliofanyika Februari 19, 2024.
“Wadau wa sekta za kiuchumi na kijamii wanashauriwa kupanga na kutekeleza shughuli zao kwa kuzingatia taarifa mahususi za hali ya hewa zinazotolewa na TMA,” amesema.
Msimu wa mvua za masika ni mahususi kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), pwani ya kaskazini (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga na visiwa vya Unguja na Pemba), ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara) na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
TMA imesema mvua za msimu zilizoanza Novemba, 2023 zimenyesha kwa kiwango cha juu ya wastani katika mikoa ya Dodoma, Singida, Kigoma, Tabora, Katavi, Iringa, Ruvuma, Lindi, Mtwara na kusini mwa mkoa wa Morogoro na wastani katika mikoa ya Rukwa, Mbeya, Songwe na Njombe katika kipindi cha Novemba, 2023 hadi Januari, 2024.
Amesema mvua hizi zilianza mapema wiki ya kwanza na ya pili ya Novemba, 2023 na zilitawaliwa na vipindi vya mvua nyingi zilizochangiwa na uwepo wa el-nino.
Katika kipindi kilichosalia cha msimu (Februari hadi Aprili, 2024), amesema mvua zinatarajiwa kuendelea kama ilivyotabiriwa Oktoba, 2023, ambapo kwa ujumla mvua zilitabiriwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani.
Kuhusu joto
Dk Chang’a amesema joto la bahari la juu ya wastani linatarajiwa katika eneo la magharibi mwa Bahari ya Hindi (pwani ya Afrika Mashariki) ikilinganishwa na upande wa mashariki mwa Bahari ya Hindi.
Vilevile, joto la bahari la chini kidogo ya wastani linatarajiwa katika eneo la kusini mwa kisiwa cha Madagascar.
“Hali hii kwa pamoja inatarajiwa kuimarisha mifumo isababishayo mvua nchini kwa kuimarisha kasi na nguvu ya msukumo wa unyevunyevu kutoka baharini kuelekea katika maeneo ya pwani ya kaskazini na nyanda za juu kaskazini-mashariki,” amesema.
Katika eneo la mashariki mwa bahari ya Atlantiki (pwani ya Angola), amesema joto la bahari la chini kidogo ya wastani linatarajiwa.
“Hali hii inatarajiwa kuimarisha msukumo wa unyevunyevu kutoka misitu ya Congo kuelekea nchini hususan katika maeneo yanayozunguka ziwa Victoria, kaskazini mwa mkoa wa Kigoma na nyanda za juu kaskazini mashariki,” amesema.
Hata hivyo, amesema hali ya El-Nino inayoendelea katika Bahari ya Pasifiki inatarajiwa kupungua nguvu hususani kuelekea mwishoni mwa msimu wa mvua za masika.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Menejimenti ya Maafa, Luteni Kanali Selestine Masalamado, amesema wamejipanga na wanaendelea kutoa elimu kwa mikoa iliyotabiriwa na kufuatilia utekelezaji wa maelekezo wanayotoa.
“Kama ambavyo tulifanya kwenye msimu wa mvua uliopita tumejipanga tuko tayari, tuna maghala ya vifaa vya kibidamu, kuna mfuko wa Taifa wa usimamizi wa maafa inapotokea tukio inaenda kusaidia.
“Tuna kamati za maafa katika ngazi zote, maghala ya vifaa vya kibinadamu katika kanda sita, mfuko wa taifa wa usimamizi wa maafa linapotokea tatizo tunakwenda kusaidia kama tulivyofanya kule Hanang,” amesema Luteni Kanali Masalamado.
Amesema pia watatoa taarifa ambayo itakuwa na maelekezo kwa sekta zote ili watambue cha kufanya pindi yatakapotokea maafa.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) Mkoa wa Dar es Salaam, Geofrey Mkinga, amesema wamejipanga kukabiliana na changamoto zozote zitakazojitokeza wakati wa mvua za masika.
“Tunatambua tuko katika kipindi cha mvua kwa hiyo kama itatokea sehemu miundombinu ikaharibika kutokana na wingi wa mvua, tutaenda kutatua changamoto kwa haraka,” amesema Mkinga.
Ametoa wito kwa wananchi kuepuka kutumia mitaro kama jalala kwa sababu maji yakisambaa itakuwa ni changamoto.
“Wananchi wasifukie mitaro kwa kumwaga taka, wahakikishe inakuwa safi muda wote tusaidiane kwa pamoja kukabiliana na hali hiyo, kwa hiyo hili ni suala la pamoja si la taasisi peke yake wakazi wa Dar es Salaam tuone kwamba tunatunza mitaro yetu na mifereji na tusiigeuze jalala,” amesema.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!