Homa kwa watoto inaashiria nini,Soma hapa kufahamu

Homa kwa watoto inaashiria nini,Soma hapa kufahamu.

VIASHIRIA VYA JOTO KALI KWA WATOTO WADOGO

Homa ya kweli inasababisha wasiwasi hasa katika miezi michache ya kwanza ya maisha ya mtoto. Hii ni kwa sababu mfumo wa kinga kwa watoto huwa bado mchanga na hauna ufanisi sana katika kupambana na maambukizi kwa miezi mitatu au minne ya mwanzo baada ya mtoto kuzaliwa.

Hivyo ni muhimu kujifunza namna sahihi ipasayo kuchukua joto la mtoto wako na kuelewa nini kinaashiria homa ya kweli.

Homa kwa mtoto

Kwa kawaida madaktari husema mtoto ana homa iwapo kama joto la mwili wake litaongezeka na kufikia nyuzijoto >37.5?? (99.5F) au zaidi.

Ni vizuri kujua joto la kawaida la mtoto wako kwa kuchukua vipimo mara chache wakati mtoto yupo katika hali ya kawaida ‘mzima wa afya’.

Nini husababisha homa kwa watoto?

Kuna sababu kadhaa ziletazo homa kwa watoto. Upungufu wa maji mwilini ni mojawapo ya sababu hizo. Aidha joto la watoto wachanga linaweza kuwa juu kufuatia nguo nyingi alizovaa katika mazingira ya joto kiasi.

Kwa kawaida inashauriwa mtoto wako avae safu moja zaidi ya mavazi zaidi ya yale ambayo wewe mwenyewe ukivaa yanakufanya ujisikie vizuri, maana yake ni kwamba kama wewe umevaa nguo mbili juu, na ukajisikia vema, basi mtoto wako avae walau nguo tatu ili kulinda joto lake lisipungue wala kuongezeka sana.

Sababu nyingine iwezayo kuleta homa kwa watoto ni maambukizi. Mfumo wa kinga ya mwili wa mtoto unapohisi kuingiliwa na vimelea vya maradhi kama vile bacteria au virusi, hutoa taarifa kwenye ubongo ambao nao hutoa kemikali fulani zinazosababisha joto kupanda mwilini.

Kupanda kwa joto huko ambako huitwa homa kunaweza kuwa na faida kadhaa katika mwilini wa mtoto zikiwemo;

Baadhi ya bakteria na virusi hawapendi hali ya joto la juu na hivyo basi ni rahisi zaidi kuharibiwa na mfumo wa kinga.

Joto la juu la mwili husaidia mwili kupambana na maambukizi.

Ni wakati gani mzazi unapaswa kuwa na hofu juu ya homa ya mtoto wako

Homa yeyote katika miezi ya mwanzo ya kuzaliwa kwa mtoto inaweza kuwa ni dalili ya kuwepo kwa maambukizi kwa mtoto, hivyo ni vizuri mtoto akafanyiwa uchunguzi wa haraka.

Watoto wote walio chini ya umri wa miezi miwili wanaopatwa na homa wanahitaji tathmini ya kina ya matibabu.

Mzazi unashauriwa kumuona daktari wa watoto kwa ajili ya uchunguzi wa kujua chanzo cha homa hiyo na matibabu zaidi. Suala hili linapaswa kufanywa angalau kwa miezi ya mitano mpaka sita ya mwanzo ya maisha ya mtoto wako.

Ieleweke kuwa homa ni dalili tu ya tatizo lililo ndani ya mwili wa mtoto. Swali muhimu zaidi la kujiuliza ni Je, mtoto wako ana hali gani? Kama mtoto wako anaonekana kuwa mgonjwa kwa njia yoyote kama vile kuwashwa, kuhangaika, uchovu, kukosa nguvu, shida ya kupumua, upele, kutapika, au kuharisha ni vyema kwa mzazi kumuona daktari wa watoto ili kujiridhisha zaidi, hata kama hali ya joto la mtoto litaonekana kuwa siyo kubwa kutosha kuitwa homa.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!