TMA yatoa angalizo la mvua kubwa siku tatu mfululizo

TMA yatoa angalizo la mvua kubwa siku tatu mfululizo

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa angalizo kwa wakazi wanaoishi ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi ukiwamo Mkoa wa Dar es Salaam, kutokana na uwezekano wa kukutana na hali mbaya ya hewa kwa siku tano na mvua kwa siku tatu mfululizo.

Maeneo mengine yaliyotajwa na mamlaka hiyo kupitia utabiri wake ni mikoa ya Tanga, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Lindi, Mtwara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na taasisi hiyo leo Jumapili, Machi 17, 2024 imesema hali hiyo itakayosababisha mvua kubwa, imetabiriwa kuanza leo hadi Machi 21 mwaka huu.

“Zingatieni na jiandaeni. Athari zinazoweza kujitokeza ni pamoja na baadhi ya makazi kuzungukwa na maji, pamoja na kuathirika kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi,” imeeleza taarifa hiyo iliyotolewa kwa umma.

Januari 20, 2024, mvua za El Nino zilinyesha na kusababisha changamoto kwa baadhi ya maeneo ikiwamo Mkoa wa Dar es Salaam.

Februari Mosi mwaka huu, mamlaka hiyo ilitoa utabiri wake ikieleza bado kuna viashiria vya mvua za El Nino hadi Aprili mwaka huu, kwa maeneo yanayopata mvua kwa msimu mmoja.

Mikoa 14 ilitajwa kukutana na hali hiyo ikiwemo, Rukwa, Katavi, Tabora, Kigoma, Singida, Dodoma , Songwe, Mbeya, Njombe, Iringa, Ruvuma, Mtwara, Lindi na Morogoro.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!