Watu 10 wafariki kwa kipindupindu Kagera
Watu 10 wafariki kwa kipindupindu Kagera
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa akizungumza wakati wa kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa huo leo Machi 6, 2024. Picha na Ananias Khalula
Ugonjwa wa Kipindupindu mkoani Kagera uligundulika Novemba 29, 2023 katika kata ya Bugorola kijiji cha Buchurago wilayani Misenyi, ambapo watu wanne walipoteza maisha, huku wengine watano wakiwahiwa matibabu.
Watu 10 wameripotiwa kupoteza maisha kwa ugonjwa wa kipindupindu tangu Novemba, 2023 hadi Machi mwaka huu, huku waliougua ugonjwa huo wakifikia 161 mkoani Kagera.
Akieleza mwenendo wa hali ya magonjwa ya mlipuko katika Mkoa wa Kagera kwenye kikao cha Kamati ya ushauri ya Mkoa (RCC) leo Jumatano Machi 6, 2024, Mkuu wa Mkoa huo, Fatma Mwassa, amesema kati ya wagonjwa wa kipindupindu 161 waliorpotiwa, 151 walipona huku 10 wakipoteza maisha.
”Kwa sasa tayari ugonjwa huu umeripotiwa katika halmashauri za Wilaya ya Missenyi, Bukoba DC na Bukoba Manispaa… mlipuko wa ugonjwa huu umeendelea kuwepo kwenye Kisiwa cha Goziba hadi tunapoongea muda huu kutokana na kuwepo kwa ugonjwa huo kwenye kisiwa hicho. Niendelee kuelekeza uongozi wa Wilaya ya Muleba kuendelea kudhibiti ugonjwa huo,”ameeleza Mwassa.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima ametaja mbinu walizozitumia kuhakikisha wanaudhibiti ugonjwa huo kwenye wilaya za Bukoba vijijini na Bukoba Manispaa kuwa ni kuhakikisha wanasimamia usafi kwenye mji mzima, kwa kuhakikisha wanazoa takataka kwenye madampo yote na yale ambayo yalikuwa siyo rasmi, kuyafunga kama vile dampoo la Kashai na dampo la Omba Mungu.
Mbunge wa Muleba kasikazini, Charles Mwijage amesema kisiwa cha Goziba kipo kwenye hatari kubwa ya kuathirika, kwa sababu ya ukosefu wa miundombinu mizuri ya maendeleo, akidai watu wanaoishi ndani ya kisiwa ni wengi, wakati eneo ni dogo hivyo kukosa huduma muhimu na za msingi kwa wakati sahihi.
Ameiomba halmashauri hiyo iwe na mikakati ya kuwanasuru wananchi wanaoishi kisiwani humo, akisema kisiwa hicho ni kati ya vyanzo vya mapato muhimu kinachozalisha zaidi ya Sh100 milioni kwa mwaka.
Via:Mwananchi.
Soma hapa Zaidi: Dalili za Ugonjwa wa kipindupindu
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!