15 wafariki, mvua zatajwa kiini, wamo watoto

15 wafariki, mvua zatajwa kiini, wamo watoto

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) David Misime.

JUMLA ya watu 15 wamefariki dunia kwa kusombwa na maji yatokanayo na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na mikoa ya Rukwa, Njombe, Manyara, Tanga, Lindi, na Lindi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo imetolewa leo Aprili 08, 2024 na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) David Misime, ambapo amesema vifo hivyo vimetokea katika nyakati tofauti kuanzia Aprili Mosi hadi Aprili 07, mwaka huu.

Msemaji huyo wa jeshi la polisi amesma kuwa kati ya watu hao 15 waliopoteza maisha, watoto ni 12 na watu wazima ni watatu.

Amesema Aprili Mosi, katika Wilaya ya Kalambo, mkoani Ruvuma, mwanaume wa miaka 18 alisombwa na maji ya mvua yalitokuwa yakitokea mlimani wakati akijaribu kuvuka daraja, huku siku hiyohiyo wilayani Kilwa, watoto wawili wenye miaka 12 nao walisombwa na maji ya mvua.

“Aprili 02, Mwanaume mwingine mwenye miaka 28 katika Wilaya ya Ludewa, mkoani Njombe naye alifariki baada ya kufukiwa na udongo ulioporopoka kutoka na mvua kubwa zilizokuwa zinanyesha mkoani humo,” amesema Kamanda Misime.

Aidha, Kamanda huyo amebainisha kuwa Aprili 03, watoto watatu kutoka katika Wilaya tofauti walifariki dunia wakati wakiogelea katika mito iliyokuwa imefurika maji ya mvua.

Kwa upande mwingine, Aprili 05, huko wilayani Babati katika mkoa wa Manyara, mwanamke mwenye miaka 55, alifariki baada ya kutumbukia kwenye shimo lenye maji.

Aidha, amesema Aprili 07, huko wilayani Kyela, mkoani Mbeya, watoto wengine watano wenye umri kati ya miaka mitano hadi sita, walifariki dunia baada ya kuzama kwenye dimbwi lililokuwa limejaa maji ya mvua wakati wanaogelea.

“Tarehe hiyohiyo mkoani Geita, watoto wengine wawili wenye umri kati ya miaka tisa na 14, walifariki kwa kusombwa na maji ya mvua yaliyokuwa yanatiririka kutoka milimani, wakati wanatoka kuokota kuni,” amesema.

Kutokana na matukio hayo, Misime ametoa wito kwa wazazi na walezi kulinda watoto kwa karibu na kuwapa melekezo sahihi kuhusiana na mvua zinazoendelea kunyesha.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!