Mafuriko yaathiri kaya 29,510 watu 125,668, Morogoro kaya 12,824 watu 51,491 na Mbeya kaya 27, 000 watu 96,000.
SERIKALI imesema wananchi 273,159 hawana makazi kutokana na mvua inayoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.
Kadhalika, viongozi wa dini wataondoka leo na treni ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam kuelekea Dodoma kwa ajili ya kufanya maombi na dua ya kuliombea taifa kesho.
Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Mobhare Matinyi, amesema jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alikuwa akizungumzia mafuriko, Muungano na safari ya majaribio ya treni ya kisasa (SGR).
Amesema idadi ya walioathirika kwa Mkoa wa Pwani ni
kaya 29,510 watu 125,668, Morogoro kaya 12,824 watu 51,491 na Mbeya kaya 27, 000 watu 96,000.
Katika maeneo ya Rufiji mafuriko yameanza kupungua kutokana na mvua kupungua katika baadhi ya mikoa ambayo mito yake huingiza maji katika Bonde la Rufiji.
Matinyi amesema kutokana na athari hizo za mvua walianzisha makazi ya muda na hadi sasa kuna kambi sita zenye waathirika 2,883 kwa Mkoa wa Pwani yenye kaya 29,510 zilizoathirika.
Amesema mvua hiyo imeathiri miundombinu ya barabara, vituo vya afya, shule, nyumba, mifumo ya maji na mashamba 152,956. 24 yenye mazao ya chakula.
Aidha, amesema misaada inaendelea kupelekwa katika mikoa ya Pwani, tani 700 za chakula, mafuta ya kula lita 7,880, vyandarua 2,260, mablanketi 1,290 na vifaa vingine ikiwamo mahema 26, magodoro 1,258, mafuta ya petroli lita 3,000 na dizeli 2,900.
Matinyi amesema mahitaji mengine kwa Mkoa wa Pwani ni boti mbili zaidi, umeme wa nguvu za jua, magodoro 2,000, vitanda 150, matangi 50 ya lita 5,000, mahema makubwa manne na madogo 10, mafuta ya petroli lita 100,000 na dizeli 50,000.
“Misaada inaendelea kuja na wahisani wanaombwa kuelekeza misaada Wilaya ya Kibiti ambapo hadi sasa kumekuwa na uhaba wa misaada kutokana na mingi kupelekwa Rufiji,” amesema Matinyi.
Amesema kwa Mkoa wa Morogoro kuna jumla ya kata 50 zilizoathirika na mafuriko na watu 78 waliokolewa na serikali. Sasa kuna kambi sita za waathirika zenye watu 1,500 na Mlimba kuna waathirika 1,365, Ifakara 135 zilizopo halmashauri mbili za Wilaya ya Kilombero.
Alisema watu wote waliopata mafuriko wapo katika makambi wanahudumiwa na serikali kwa kupewa chakula, makazi, tiba, maji na usalama.
Matinyi amesema tathimini ya mafuriko ya mvua inaendelea kufanywa na watatoa taarifa ikiwamo idadi kamili ya vifo vilivyotokana na mafuriko ya mvua.
Aidha, amesema viongozi wa dini, watendaji wa serikali, watumishi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) na waandishi wa habari baada ya kumaliza ibada kesho watapanda treni hiyo majira ya saa nane mchana na kuwasili Dar es Salaam majira ya saa moja usiku.
Amesema treni hiyo ipo katika majaribio, na isije kuonekana imetumia muda mrefu kusafiri. “Hizi ni shughuli za majaribio mwendokasi sio kipimo cha kazi haya ni majaribio.”
Amesema hadi sasa wameshapokea mabehewa ya treni ya kisasa 65 na vichwa tisa “kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro kimekamilika kwa asilimia 98.9 na kipande cha Morogoro kwenda Dodoma kimekamilika kwa asilimia 96.1.”
Amesema nchi inaadhimisha miaka 60 ya Muungano na kumekuwa na matukio mbalimbali ya kuzindua mradi, tukio kubwa linalofuata Aprili 22, mwaka huu jijini Dodoma ni kuliombea taifa na mgeni rasmi ni Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango.
Amesema wananchi wataanza kuingia katika uwanja kuanzia saa 12 asubuhi kutakuwa na burudani mbalimbali ikiwamo kwaya na shughuli la kuliombea taifa itaongozwa na viongozi wa dini.
Amesema tukio jingine kubwa ni Aprili 24, mwa huu kutakuwa na uzinduzi wa kitabu cha miaka 60 ya historia ya Makamu wa Rais iliyoanzishwa baada ya Muungano kutokea.
Aidha, amesema Aprili 25, majira ya saa tatu Rais Samia Suluhu Hassan, atalihutubia taifa kutoa ujumbe wa maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano saa sita kamili usiku, mikoa ya Arusha, Dodoma, Dar es Salaam, Geita, Mbeya, Mwanza na Zanzibar kutakuwa na urushwaji wa fataki.
Amesema Aprili 26, kilele cha shughuli hizo zitafanyika katika kiwanja cha Uhuru na mgeni rasmi atakuwa Rais Samia.
Taifa linatarajia kuwa na wageni kutoka mataifa ya jirani na marafiki katika siku hiyo.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!