Shirika la Afya Duniani WHO Laingiza zaidi ya tani 50 za vifaa vya matibabu Sudan

Shirika la Afya Duniani WHO Laingiza zaidi ya tani 50 za vifaa vya matibabu Sudan

#PICHA; Vifaa vya matibabu vinatayarishwa kwa ajili ya kupelekwa kwenye Milima ya Blue Nile na Nuba nchini Sudan.

Shirika la Afya Ulimwenguni WHO limefanikiwa kuwasilisha zaidi ya tani 50 za vifaa vya matibabu kwa mikoa ya Blue Nile na Milima ya Nuba nchini Sudan, ambayo inatarajiwa kuhudumia takriban watu 830,000 katika muda wa miezi mitatu ijayo.

Mzozo unaoendelea nchini Sudan umetatiza kwa kiasi kikubwa uwezo wa ofisi ya WHO Sudan kupata na kupeleka vifaa muhimu vya matibabu vya dharura katika mikoa ya Blue Nile na Milima ya Nuba iliyoko kusini mwa Kordofan.

Katika kukabiliana na hali hiyo, ofisi hiyo ilishirikiana na mwenzake wa nchi jirani ya Sudan Kusini wamefanikiwa kuwezesha uwasilishaji wa vifaa hivyo vya msingi, kwani ofisi ya shirika hilo nchini Sudan Kusini ilihifadhi kiasi kinachohitajika katika maeneo yanayopakana na mpaka wa Sudan kwa ajili ya maandalizi ya kusafirisha kuelekea katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro.

Mwakilishi wa WHO nchini Sudan Kusini, Dk. Humphrey Karamaji alisema, “Kwa vile ugavi una jukumu muhimu katika kukabiliana na dharura, lazima tuwe na uwezo mkubwa wa vifaa ili kuhakikisha usambazaji wa haraka wa vifaa kwenye maeneo yaliyoathirika.”

Vifaa hivyo vilivyopelekwa nchini Sudan vilijumuisha vifaa vya afya vya dharura, vifaa vya uchunguzi na matibabu ya kipindupindu, vifaa vya kudhibiti surua na magonjwa yasiyoambukiza, matatizo ya kiafya yanayohusiana na utapiamlo mkali kwa watoto walio chini ya miaka mitano, na kiwewe cha dharura na vifaa vya upasuaji.

Ikumbukwe kuwa hii ni mara ya pili kwa ofisi ya shirika hilo nchini Sudan Kusini kuweza kupeleka msaada nchini Sudan tangu kuzuka kwa mzozo mwezi Aprili 2023.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!