Upasuaji kwa njia ya tundu dogo wa kurekebisha mishipa ya damu iliyotanuka wafanyika
Upasuaji kwa njia ya tundu dogo wa kurekebisha mishipa ya damu iliyotanuka wafanyika
Kwa mara ya kwanza wataamu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) wamefanya upasuaji kwa njia ya tundu dogo wa kurekebisha mishipa ya damu iliyotanuka na kupasuka sehemu ya kifua na tumbo kwa wagonjwa watano wenye matatizo hayo.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema wagonjwa wenye matatizo hayo wengi wao walikuwa wakipoteza maisha na wale ambao walikuwa wanapona walipewa rufaa ya kwenda kutibiwa nje ya nchi.
Dk Kisenge alisema upasuaji huo umefanywa na madaktari wazawa kwa kushirikiana na madaktari kutoka India na tayari mgonjwa mmoja alishafanyiwa upasuaji huku wengine watatu watafanyiwa upasuaji huo leo na mmoja kesho.
“Kwa mara ya tatu tunavunja rekodi tumefanya matibabu makubwa ya kurekebisha mishipa ya damu ambayo imetanuka na kupasuka hii ni tatizo ambalo watu wengi wanalipata na kupoteza maisha ghafla na wanaobaki tunawapeleka nje ya nchi lakini hivi sasa tutaanza kuwahudumia hapa nchini”,.
“Ni upasuaji mkubwa kufanyika Tanzania na Afrika Mashariki na Kati tumevunja rekodi tunampongeza Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapenda wananchi wake na kutoa kiasi cha shilingi milioni 900 za matibabu ya kibingwa katika Taasisi yetu,”, alisema Dkt. Kisenge.
Mkurugenzi huyo Mtendaji ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema mishipa ya damu ya tumboni na kifuani kutanuka na kupasuka kunasabahishwa na vitu vingi ikiwemo shinikizo la juu la damu ambayo haitibiwi vizuri,uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe uliokithiri na uzito mkubwa.
Dkt. Kisenge alisema katika Taasisi hiyo kuna wagonjwa wapatao 30 wanaosubiri kupata matibabu hayo ambapo gharama zake ni shilingi milioni 80 endapo mgonjwa atatibiwa hapa nchini na milioni 150 akitibiwa nje ya nchi.
“Tutaendelea kutoa matibabu haya na tutaendelea kuwa na matibabu mapya mengine kwani wataalamu wetu wanajifunza kila siku. Upasuaji huu tulioufanya ukifanyika kwa njia ya kufungua kifua unachukua saa nane ila kwa njia ya tundu dogo ni saa mbili hii ni njia nzuri japo gharama ni kubwa ila Mhe. Rais wetu ametoa fedha ili wananchi wasaidiwe”, alisema Dkt.Kisenge.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!