Watoto wa kike milioni 5 nchini Tanzania kupatiwa chanjo dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi- WHO

Watoto wa kike milioni 5 nchini Tanzania kupatiwa chanjo dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi- WHO

#PICHA: Uzinduzi wa kampeni ya siku 5 ya kitaifa ya chanjo dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi nchini Tanzania uliambatana na wanawake na wanaume kubeba mabango yenye ujumbe kuhusu usalama wa chanjo hiyo.

Nchini Tanzania kampeni ya siku 5 ya chanjo dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi, au Human Papilloma Virus, (HPV) imeingia siku ya tatu hii leo nchini kote ikilenga zaidi ya watoto wa kike milioni 5 wenye umri wa kati ya miaka 9 hadi 14.

Taarifa iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni huko jijini Geneva, nchini Uswisi na Mwanza nchini Tanzania inasema kampeni hiyo inaendeshwa kwa ubia kati ya serikali ya Tanzania,  Ubia wa chanjo duniani, GAVI , mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la kuhudumia watoto UNICEF na WHO.

Virusi vya HPV ni sababu kuu ya saratani ya shingo ya kizazi, kwingineko ikijulikana kama mlango wa kizazi au Cervical Cancer kwa lugha ya kiingereza na kampeni itamalizika tarehe 26 mwezi huu wa Aprili.

WHO inasema wakati saratani ya shingo ya kiazi inasalia kuwa moja ya sababu kuu ya vifo miongoni mwa wanawake nchini Tanzania, ambapo mwaka 2022 wagonjwa 6,800 kati ya 10,800 walifariki dunia, bado ugonjwa huo unazuilika kwa chanjo.

“Chanjo ya HPV ni salama na ina ufanisi mkubwa katika kuzuia maambukizi,” inasema WHO, ikiongeza kuwa wakati wa kampeni, watoto wa kike wenye umri wa kupatiwa chanjo hiyo watakuwa na fursa ya kupatiwa dozi moja ya chanjo bila gharama yoyote.

Muuguzi nchini Tanzania akimpatia mtoto wa kike chanjo dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi, au HPV wakati wa uzinduzi wa kampeni ya siku 5 ya chanjo hiyo kwenye taifa hilo la Afrika Mashariki.

Utoaji wa chanjo ya HPV Tanzania umekuwa wa mafanikio

Shirika hilo linaongeza kuwa juhudi za kuongeza upatikanaji wa chanjo hiyo dhidi ya saratani nchini kote Tanzania zimekuwa na mafanikio makubwa.

Mwaka 2018, chanjo hiyo inayotolewa kwa dozi mbili, ilijumuishwa kwenye programu ya chanjo ya kitaifa kwa watoto wote wa kike wenye umri wa miaka 14, ikionesha azma ya serikali ya Tanzania ya kulinda afya na ustawi wa vizazi vijavyo.

Hali leo hii, kwa mujibu wa WHO, ufikiaji wa dozi ya kwanza ya HPV ni asilimia 79, na dozi ya pili asilimia 60.

Ni kwa kuzingatia hilo, WHO inasema juhudi za pamoja zinahitajika kuhakikisha kila mtoto wa kike Tanzania anapata kinga hiyo muhimu dhidi ya ugonjwa huo hatari lakini wenye kinga.

Maendeleo ya Tanzania katika kutoa chanjo ya HPV ni muhimu kama sehemu ya mpango wa kimataifa unaoungwa mkono na Ushirika wa Chanjo ambao umeazimia kutoa fedha zaidi na rasilimali ili kuhakikisha watoto wa kike milioni 86 kote duniani wanakuwa wamepatiwa chanjo hiyo ifikapo mwaka 2025.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!