Wiki ya Kimataifa ya Chanjo yaanza leo 24 hadi 30 Aprili
Wiki ya Kimataifa ya Chanjo ambayo huadhimishwa katika kila wiki ya mwisho ya mwezi Aprili, inalenga kuangazia hatua za pamoja zinazohitajika na kuhimiza matumizi ya chanjo kuwalinda watu wa rika zote duniani dhidi ya magonjwa.
Shirika la Afya Duniani, WHO linashirikiana na nchi kote ulimwenguni kuhamasisha ufahamu wa thamani ya chanjo na uchanjaji na kuhakikisha kuwa serikali zinapata mwongozo unaohitajika na usaidizi wa kiufundi ili kutekeleza programu za uchanjaji zenye ubora wa hali ya juu.
Lengo kuu la Wiki ya Kimataifa ya Chanjo ni kwa watu zaidi na jamii zao kulindwa dhidi ya magonjwa yanayoweza kuzuilika.
WHO inasema chanjo zimesaidia sana ikitolea mfano namna ulimwengu umeweza kutokomeza ugonjwa wa ndui ambapo mtu wa mwisho kuugua ugonjwa huo ni miaka 47 iliyopita.
Mwaka huu Wiki ya Kimataifa ya Chanjo inaadhimisha miaka 50 ya EPI ambao ni mpango ambao WHO iliuanzisha mwaka 1974 kwa lengo la kufanya chanjo zipatikane kwa watoto wote duniani.
WHO inatoa wito kwa nchi kote duniani kuongeza uwekezaji katika mipango ya chanjo ili kulinda vizazi vijavyo.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!