ZAIDI ya kaya 2,500 katika Kata ya Muhoro, wilayani Rufiji, mkoani Pwani zimeathiriwa na mafuriko

ZAIDI ya kaya 2,500 katika Kata ya Muhoro, wilayani Rufiji, mkoani Pwani zimeathiriwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.

Imeelezwa kuwa mafuriko hayo yamesababisha zaidi ya wananchi 10,000 kukosa mahali pa kuishi.

Diwani wa Muhoro, Abdul Chobo, akizungumza na Nipashe kwa simu jana, alisema mafuriko hayo yamewaacha katika hali ngumu kwa kuwa wengi wao hawana mahali pa kushi, huku mali na mashamba yao yakiharibiwa na maji.

Alisema kata yake ina vijiji sita na vitongoji 27. Kati ya vitongoji, viwili ndivyo havijakumbwa na maafa, lakini vilivyosalia vimeathiriwa.

Alisema wananchi waliokosa makazi kutokana na mafuriko ni wengi, wakihifadhiwa shuleni na wengine kupata hifadhi kwa ndugu.

“Kuna baadhi ya shule za msingi zimezingirwa na maji. Kwa mfano, Shule ya Msingi Muhoro imefungwa na nyingine wataalamu wanaendelea kufanya tathmini kuona kama zitafungwa au la.

“Kuna watoto wa sekondari wanaohitaji kuvuka maji ili wafike shuleni na kurudi majumbani, lakini wameshindwa kutokana na mafuriko. Wananchi wengi wamepoteza mazao, mashamba na mifugo yao,” alisema diwani huyo.

Chobo alisema kuwa awali Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) ilitahadharisha na kuwataka kuchukua hatua za kuhama, lakini wengine walipuuza ingawa kuna wachache waliochukua hatua na wameepuka madhara hayo.

Alisema kutokana na mvua ilivyokuwa inanyesha kwa wingi, walitarajia kupata mafuriko hayo tangu Desemba mwaka jana, lakini kuwapo Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), kumesaidia kuzuia athari zaidi.

Hata hivyo, kuna dhana kwamba kufunguliwa kwa milango ya bwawa hilo kumesababisha hali inayoshuhudiwa sasa Rufiji.

“Hatuwezi kusema bwawa limesababisha mafuriko, si mara ya kwanza kutokea. Mara ya mwisho yalitokea mwaka 2020. Je, kulikuwa na bwawa? Je, na yale yaliyotokea mwaka 1978 na 1998 yalisababishwa na bwawa? Kwahiyo, bwawa si sehemu ni matokeo ya mvua kubwa na asili ya Rufiji,” alisema.

Diwani huyo alisema kilio kikubwa kwa sasa ni chakula na makazi mengine ya dharura, ili waliothiriwa wapate mahali pa kujisitiri huku wakisubiri hatua za serikali.

Pia aliomba huduma za afya zisogezwe haraka walioko wananchi hao ili kuepuka magonjwa ya mlipuko, akifafanua kwamba kutokana na mafuriko hayo, vyoo vingi vimezibuka na hivyo wanakijiji wengi wapo katika hatari ya kupata magonjwa ya mlipuko.

Alipoulizwa kuhusu hatua zilizochukuliwa na serikali mpaka sasa, diwani huyo alisema kuwa kwa mujibu wa mkuu wa wilaya, ofisi ya waziri mkuu imetoa mahindi tani 20 na wahisani mbalimbali wameanza kuchangia misaada ya chakula.

“Serikali, viongozi wa chama, wilaya na mkoa wamefika, timu za wataalamu wa takwimu na sasa mkuu wa wilaya anaendesha kikao kuona kinachopatikana kinawafikia walengwa,” alisema.

Mwenyekiti wa Kijiji Cha Muhoro Magharibi ambacho kimeathiriwa na mafuriko hayo, Amina Mnyimwa aliomba serikali ipeleke msaada wa chakula haraka.

Alisema tani zinazohitajika ni nyingi kwa kuwa walioathirika na mafuriko katika kata hiyo ni zaidi ya 16,000.

“Watu wakipata chakula watatulia, kilio kingine ni mazao yao mengi yamepotea, watu wangekuwa wanakula ndizi, mpunga ungekuwa tayari umekomaa, mahindi, ufuta hali ni mbaya sana,” alilalama mwenyekiti huyo.

Jana Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) lilitoa taarifa kwa umma, likisema: “Bwawa la JNHPP limesaidia kupunguza athari za mafuriko. Sababu kubwa ya mafuriko kwenye wilaya za Kibiti na Rufiji ni kuongezeka mtiririko wa maji katika Mto Rufiji kulikosababishwa na mvua kubwa za El-Nino zinazoendelea kunyesha katika mikoa ya nyanda za juu kusini.”

Mjumbe wa Kamati Kuu Taifa Chama Cha ACT Wazalendo, Husna Sungura alisema ni muhimu serikali ikachukua hatua za haraka kusaidia waathirika wa mafuriko hayo.

“Wanawake na watoto wanateseka sana, kinamama biashara zimekufa, watoto hawaendi shuleni, wananchi tunalipa kodi, sasa hizo kodi zetu matumizi yake ni wapi kama watu wanapata maafa na hawana pa kukimbilia?” Husna alihoji.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!