Kwa mujibu wa WHO, ni karibu theluthi moja tu ya hospitali 36 zilizoko Gaza ndizo ambazo bado zinafanya kazi

#PICHA:Mama na bintiye wanapokea huduma katika Hospitali ya Kamal Adwan kaskazini mwa Gaza mnamo Aprili 2024.

Huku mashambulizi ya mabomu yanayofanywa na jeshi la Israel yakiendelea usiku kucha katika Ukanda wa Gaza, pamoja na uvamizi wa ardhini na mapigano makali, mkuu wa Shirika la Umoja La Afya duniani WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus ametoa tahadhari hii leo kwa wafanyakazi na wagonjwa katika hospitali iliyozingirwa ya Al-Awda iliyoko kaskazini mwa Gaza.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X Dkt.Tedros amesema kuwa “Wahudumu wa afya ndani ya hospitali waliripoti shambulio mnamo tarehe 20 Mei, na washambuliaji wakilenga jengo na roketi ya risasi ikigonga ghorofa ya tano,”

Takriban wafanyakazi 148 na wagonjwa 22 na watu wanao wauguza wenzao wamesalia “wamekwama ndani” ya hospitali hiyo tangu Jumapili, Mkurugenzi Mkuu wa WHO aliongeza, kabla ya kutoa ombi la watu hao kupatiwa ulinzi.

WHO ikipeleka vifaa muhimu vya matibabu wakati ujumbe wa Umoja wa Mataifa wakiwa katika hospitali ya Al-Awda kaskazini mwa Gaza mapema mwaka huu. (Maktaba)

Athari ya agizo la watu kutakiwa kuondoka

Kwa mujibu wa WHO, ni karibu theluthi moja tu ya hospitali 36 zilizoko Gaza ndizo ambazo bado zinafanya kazi, na hali hiyo imeacha vituo vya huduma muhimu vya afya “kutoweza kufikiwa” na wagonjwa na wafanyakazi wa afya walioathiriwa na ghasia au maagizo ya kuhama.

WHO wamebainisha kuwa katika mji wa kusini wa Rafah, amri za jeshi la Israel kuwaambia Wagaza wahame zimeathiri zaidi ya vituo 20 vya matibabu, hospitali nne na vituo vinne vya afya ya msingi.

Kaskazini mwa Gaza, wakati huo huo, vituo 16 vya matibabu vimeathiriwa na vile vile vituo vitano vya afya ya msingi na Hospitali ya Kamal Adwan, pamoja na Hospitali ya Al-Awda.

Katika chapisho lake kwenye mtandao wa kijamii wa X siku ya Jumapili, Dkt.Tedros alitoa wasiwasi wake kuhusu ripoti za uhasama mkali katika eneo la Hospitali ya Kamal Adwan pamoja na mmiminiko wa wagonjwa waliojeruhiwa licha ya uwezo mdogo wa kuwatibu.

Takriban watu 900,000 wa Gaza wameondolewa

Katika tukio linalohusiana na hilo, ofisi ya uratibu wa misaada ya Umoja wa Mataifa, OCHA, iliripoti kwamba operesheni inayoendelea ya kijeshi ya Israel na amri za kuwahamisha watu zimeng’oa zaidi ya watu 900,000 katika wiki mbili zilizopita – hii ni sawa na watu waGaza wanne kati ya 10.

Hii inajumuisha watu 812,000 kutoka Rafah na wengine zaidi ya 100,000 kaskazini mwa Gaza, huku mamia kwa maelfu wakipitia hali mbaya ya maisha.

“Wadau wa kibinadamu wanaofanya kazi ya kutoa msaada wa makazi kwa watu huko Gaza wanaripoti kwamba hakuna hema na vifaa vichache sana vya makazi vilivyosalia kwa usambazaji,” OCHA ilisema.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!