Ticker

6/recent/ticker-posts

TMA yataja chanzo cha mvua zinazonyesha kwa Sasa,baadhi ya maeneo



TMA yataja chanzo cha mvua zinazonyesha kwa Sasa,baadhi ya maeneo

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema, mvua zinazoendelea kunyesha tangu jana katika baadhi ya mikoa nchini zimetokana na kuongezeka kwa joto la bahari magharimbi mwa Bahari ya Hindi katika mwambao wa pwani wa nchi.

Mvua hizo ziliibua sintofahamu kutokana na majira ya Juni kuwa ya kipupwe, huku TMA ikitaja mikoa ambayo inapata mvua hizo.

Mikoa hiyo ni yote  ya ukanda wa Pwani,ukanda wa ziwa Victoria kwenye mikoa ya Kagera, Simiyu, Geita na Mara na maeneo ya Nyanda za juu Kaskazini Mashariki katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara na Kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.

Meneja wa Utabiri wa TMA, Dk Mafuru Kantamla leo Jumatano Juni 19, 2024 ameiambia Mwananchi Digital kwamba mvua hizo hazina madhara.

“Ni mvua za kawaida, kama itatokea mifumo ikasoma zitakuwa na madhara pia tutasema, watu waendelee kufuatilia utabiri kwa kuwa mifumo inapoimarika zaidi ndipo kunasababisha mvua kuwa nyingi kidogo, kwa sasa mifumo inaonyesha mvua hizi hazina madhara,” amesema.

Amesema, kwenye ukanda wa pwani mvua zitayesha leo Juni 19 na kesho Juni 20 kisha itapungua na vipindi vya jua vitaendelea kama kawaida baada ya siku hizo mbili.

“Hata mikoa mingine, si kama zitakuwa na muendelezo, mifumo inaonyesha ni za kutafuta na ilionekana katika msimu huu wa kipupwe pamoja na kuwa na vipindi vya ukavu na upepo mkali, kutakuwa na mvua kutokana na kuongezeka kwa joto Magharibi mwa Bahari ya Hindi.” amesema.



Post a Comment

0 Comments