Homa ya Ini janga kwa Dunia,Takwimu mpya Zaonyesha

TAKWIMU za homa ya ini duniani zinaonesha zaidi ya watu milioni 240 huugua. Tanzania, watu watano hadi wanane kati ya 100 wanaugua ugonjwa huo, hususan aina ya B na C.

Bingwa wa Magonjwa ya Ini na Mfumo wa Chakula kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila, Dk. Tuzo Lyuu, amebainisha hayo jana, jijini Dar es Salaam, katika maadhimisho ya Siku ya Homa ya Ini Duniani, ambayo huadhimishwa Julai 28, kila mwaka.

Tovuti ya Umoja wa Mataifa (UN), kwenye maadhimisho hayo jana, imebainisha kwamba homa ya ini inaua takribani watu 3,500 kila siku licha ya kuwapo kinga na tiba, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

WHO inasema kiungo hicho kina shughuli zaidi ya 500 kila siku, kuhakikisha binadamu anaendelea kuishi, likisisitiza umuhimu wa kuchunguza, kutibu na kuzuia virusi vya homa ya ini.

Akifafanua kuhusu ugonjwa huo, Dk. Lyuu alisema kwa kawaida mwili hupambana na ugonjwa huo, iwapo ni homa ya ini aina ya A na E.

“Kuna aina ya homa ya ini katika makundi haya; virusi vya hepatitis A na E na hepatitis B na C. Ugonjwa huu maambukizi yake aidha ni kwa njia ya kujamiiana bila kinga, kuongeza damu ya mwenye homa hii au kwa njia ya mdomo yaani chakula.

Hata hivyo, maambukizi yanaweza kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito. Homa ya ini aina ya A na E huwa haiwi ‘chronic’ (sugu) na haikai muda mrefu mwili hupambana wenyewe ila wapo ambao hushindwa kupambana,” alisema bingwa huyo.

Alisema kuwa homa ya ini ya hepatitis B na C ndiyo hatari na maambukizi hukaa muda mrefu mwilini na yenye kuambukiza zaidi na kwamba duniani takribani watu 650,000 hupoteza maisha kutokana na homa hiyo.

Dalili za homa hii ni kutapika, macho kuwa ya njano, tumbo kuvimba. Madhara yake ni uvimbe katika ini au kupata saratani. Mabadiliko ya ini kusinyaa na kushindwa kufanya kazi,” alisema bingwa huyo.

Kuhusu tiba bingwa huyo alisema anayeugua homa aina C, inashauriwa aanze tiba ambayo kwa asilimia zaidi ya 95 ya wanaotumia dawa wanapona.

WHO

WHO inasema chanjo wakati wa utotoni, hupunguza kwa kiasi kikubwa maambukizi sugu na visa vya saratani ya ini na cirrhosis katika utu uzima.

“Ni wakati wa kuchukua hatua, kila sekunde 30 mtu mmoja anafariki dunia kutokana na ugonjwa unaohusiana na homa ya ini.

Lazima kuchagiza hatua bora za kinga, uchunguzi na tiba ili kuokoa maisha na kupata matokeo bora ya afya.”

WHO, kimataifa kuna aina tano za Homa ya Ini za virusi vinavyosababisha homa ya ini A, B, C, D na E. Kwa ujumla, maambukizi ya homa ya ini aina ya B na C ndio yamesambaa zaidi na husababisha vifo vya watu milioni 1.3 kila mwaka na maambukizi mapya kwa watu milioni 2.2 kila mwaka.

Licha ya kuwapo kwa mbinu bora za uchunguzi na matibabu na kupungua kwa gharama za huduma hizo, viwango vya uchunguzi na matibabu vimedorora, linasema WHO.

Shirika hilo linaona dunia ina nafasi ya kufikia viwango vya kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030, iwapo hatua zitachukuliwa mapema hivi sasa.

“Watu 6,000 huambukizwa homa ya ini B na C kila siku. Vifo vinavyosababishwa na virusi vya homa ya ini vinaongezeka. Mwaka 2022 homa ya ini aina B na C vilisababisha vifo vya watu milioni 1.3.”

Serikali yataka wazazi kuzingatia chanjo kwa watoto

UMUHIMU CHANJO

Serikali imewataka wazazi kuwapa chanjo watoto wao wanapozaliwa ili kuwakinga na maradhi ya kuambukiza ikiwamo homa ya ini.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk. Grace Magembe, aliyasema hayo jana katika maadhimisho ya Siku ya Homa ya Ini kitaifa yaliyofanyika mkoani Dar es Salaam yakiwa na lengo la kuongeza uelewa wa tatizo hilo.

Aliwakumbusha wazazi hao kutotoka hospitali bila watoto wao kupatiwa chanjo, akieleza kwenye chanjo hizo ipo ya homa ya ini na inamkinga na maambukizi ya ugonjwa huo.

Aidha, serikali ilijumuisha chanjo hiyo tangu mwaka 2002 kwenye chanjo inayojulikana kitaalam kama ‘pentavalent vaccine’ wanayopatiwa watoto chini ya miaka mitano kuwaweka salama dhidi ya virusi hivyo.

Aliwapongeza Watanzania wanaojitokeza kuchangia damu na kuwahamasisha wengine kuunga mkono kwa kuwa inasaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wanayoihitaji ikiwamo homa ya ini, Ukimwi, saratani na waliopata ajali.

Alisema uchangiaji damu pia husaidia serikali kuitambua hali ya maambukizi ya magonjwa hayo kwa kuwa inakwenda kupimwa kuangaliwa usalama kabla ya kuwekewa mgonjwa.

Alisema utekelezaji wa utoaji chanjo ya homa ya ini inatokana na Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi na Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini (NASHCoP), uliozinduliwa na wizara ya afya Novemba, mwaka jana.

Alisema magonjwa mengi yanaweza kuzuilika iwapo Watanzania watapata taarifa sahihi wanapokwenda kufuata huduma.

Watanzania pia wamekumbushwa kuzingatia matumizi sahihi ya dawa na kula milo sahihi kwa kuwa magonjwa mengine ya ini yanatokana na matumizi mabaya ya vitu hiyo pamoja na kemikali.

Mkuu wa Programu wa Wizara ya Afya, Dk. Catherine Joachim, alisema kwa mara ya kwanza nchi hiyo inafanya maadhimisho ya kitaifa ya ugonjwa huo toka mpango wa NashCop ulipazinduliwa Novemba 24, 2023.

Alisema tangu walipoanza kutoa huduma ya kupima ugonjwa huo Julai 25, mwaka huu, idadi ya waliojitokeza kupima hadi kufikia juzi ni 524, kati ya hao 15 sawa na asilimia 2.8 waligundulika kuwa na maambukizi, ambao ipo chini ya kiwango cha ushamiri cha kimataifa ambao ni asilimia tatu.

Watu 429 walipokea chanjo ya kwanza na kuunganishwa na vituo vingine ili wapate chanjo mbili zilizobakia, jumla ya chupa 26 za damu zilikusanywa kutoka kwa wachangiaji na watu 275 walipatiwa huduma ya ukatili wa kijinsia na 114 walipata huduma ya macho.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!