Homa ya ini yaua watu 3,500 kila siku licha ya kuweko kinga na tiba- WHO

Homa ya ini yaua watu 3,500 kila siku licha ya kuweko kinga na tiba- WHO

Kuzuia maambukizi ya homa ya ini kwa njia ya chanjo za utotoni hupunguza kwa kiasi kikubwa maambukizo sugu na visa vya saratani ya ini na cirrhosis katika utu uzima.

Leo Julai 28 ni siku ya kimataifa ya kuelimisha umma kuhusu homa ya ini au Hepatitis, ambapo ini linavimba na kusababisha ugonjwa mkali wa ini na saratani.

Ni wakati wa kuchukua hatua, ndio ujumbe mahsusi wa siku hii ya leo kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO kwani shirika hilo linasema kila sekunde 30 mtu mmoja anafariki dunia kutokana na ugonjwa unaohusiana na homa ya ini.

Hivyo WHO inasema lazima kuchagiza hatua bora za kinga, uchunguzi na tiba ili kuokoa maisha na kupata matokeo bora ya afya.

Aina 5 za Homa ya Ini

Kuna aina 5 za virusi vinavyosababisha homa y aini – A, B, C, D na E. Kwa ujumla, maambukizi ya homa ya ini aina ya B na C ndio yamesambaa zaidi na husababisha vifo vya watu milioni 1.3 kila mwaka na maambukizi mapya kwa watu milioni 2.2 kila mwaka.

Licha ya kuweko kwa mbinu bora za uchunguzi na matibabu na kupungua kwa gharama za huduma hizo, viwango vya uchunguzi na matibabu vimedorora, inasema WHO.

Ingawa hivyo bado shirika hilo linaona dunia ina nafasi ya kufikia viwango vya kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030, iwapo hatua zitachukuliwa mapema hivi sasa.

Ujumbe muhimu mwaka 2024

Majukumu ya ini kila siku ya ini

Ini lina shughuli zaidi ya 500 kila siku za kuhakikisha binadamu anaendelea kuishi, na ndio maana WHO inasisitiza umuhimu wa kuchunguza, kutibu na kuzuia virusi vya homa ya ini.

Watu 6,000 huambukizwa homa ya ini B na C kila siku

Vifo vinavyosababishwa na virusi vya homa ya ini vinaongezeka. Mwaka 2022 homa ya ini aina B na C vilisababisha vifo vya watu milioni 1.3. Takribani watu milioni 304 wanaishi na maambukizi sugu ya homa ya ini. Watu 3,500 wanakufa kutokana na homa ya ini aina ya B na C kila siku, sawa na mtu mmoja kila baada ya sekunde 30. Na kwa maambukizi, zaidi ya watu 6,000 wanaambukizwa virusi vya homa ya ini kila siku.

Kuna idadi kubwa ya wagonjwa wa homa ya ini wasiojitambua

WHO inasema duniani kote takribani watu milioni 220 wana homa ya ini aina ya B lakini hawajui, ilihali kwa aina ya C watu milioni 36 wameambukizwa virusi lakini hawajui.

Dalili nyingi hutokea pale ambapo ugonjwa uko hatua za mwisho, hasa pale mtu ameshapata ugonjwa wa ini au saratani.

Hata baada ya mgonjwa kubainika na homa ya ini, kiwango cha matibabu na huduma bado ni kidogo.

Kati ya watu milioni 304 wenye homa ya ini aina ya B na C, ni milioni 7 tu wanatibiwa aina ya B na milioni 12.5 aina ya C.

Maambukizi na vifo vinaweza kuzuiwa

Ili kutokomeza homa ya ini na kufikia lengo la WHO mwaka 2030, hatua rahisi za huduma kudhibiti ugonjwa huo ni pamoja na; wajawazito wote wanaoishi na homa ya ini sugu aina ya B wapatiwe tiba na watoto wao wapatiwe chanjo dhidi ya ugonjwa huo ili kuzuia maambukizi.

Halikadhalika asilimia 90 ya watu wenye maambukizi ya homa ya ini B na C wapatiwe matibabu.

Kufahamu zaidi kuhusu homa ya ini (Hepatitis) na dalili zake bofya hapa.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!