Kanda ya Afrika inakumbana na ongezeko kubwa la wagonjwa wa mpox tangu mwanzo wa mwaka huu 2024, huku nchi nyingi zilizokuwa hazijaathirika na ugonjwa huu zikiripoti kusambaa kwa virusi vya ugonjwa huo.
Akizungumza leo kutoka mjini Brazzaville, Jamhuri ya Congo, Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni WHO kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moeti, amesema “kipaumbele chetu ni kukomesha maambukizi ya virusi hivyo kwa haraka. Tunashirikiana na washirika wetu kusaidia nchi kuimarisha hatua za kudhibiti mlipuko na kuhakikisha kwamba jamii zinashiriki kwa kiasi kikubwa katika juhudi za sasa za kumaliza milipuko hii kwa ufanisi.”
Taarifa hiyo pia imethibitisha kwamba nchi kumi na tano za Afrika kwa sasa zinaporipoti mlipuko wa mpox, huku jumla ya wagonjwa 2030 wakithibitishwa na vifo 13 kufikia sasa mwaka huku nchi za Burundi, Kenya, Rwanda, na Uganda zikiripoti wagonjwa tangu katikati ya Julai 2024.
Maambukizi ya Mpox
Kwa mujibu wa WHO Mpox husambazwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, ambapo waathirika wengi hupatikana karibu na misitu ya mvua za kitropiki ambako kuna wanyama wanaobeba virusi. Ugonjwa huu pia unaweza kuenea kutoka kwa binadamu hadi binadamu kupitia kuugusa umajimaji wa mwilini, vidonda kwenye ngozi au ndani ya mwili, kama kinywani au kwenye koo, matone yatokanayo na kupumua au vitu vilivyochafuliwa.
Kulingana na taarifa hiyo, aina mpya iliyotokea mnamo Septemba 2023 inazunguka katika eneo la mashariki la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambako kuna zaidi ya asilimia 90 ya kesi zilizoripotiwa.
Vilevile ripoti hio imebaini kuwa Rwanda na Uganda wameripoti kesi za aina hii mpya, huku Kenya ikithibitisha wagonjwa wa aina hii mpya.
Kuhusu Burundi, taarifa inaeleza kuwa uchambuzi unaendelea nchini humo ili kubaini kama kesi zilizoripotiwa zinahusiana na aina hii mpya.
Dkt. Moeti pia alibaini kwamba mwenendo wa maambukizi unatofautiana katika kanda, huku kuenea kwa aina mpya inayojulikana kama clade 1b mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ikihusishwana maambukizi kupitia mawasiliano ya kingono na uhamaji mkubwa wa watu, wakati nchini Afrika Kusini, wagonjwa wengi ni miongoni mwa wanaume wanaoshiriki ngono na wanaume wenzao.
Dkt. Moeti ameleeza kuwa ingawa maambukizi Afrika Magharibi na Kati yanahusishwa na mlipuko wa kimataifa wa mwaka 2022, uchambuzi zaidi unahitajika ili kuelewa vizuri mifumo ya maambukizi na kuboresha hatua dhidi ya mlipuko.
WHO inashirikiana na nchi husika
Taarifa hio pia imebaini kwamba WHO inafanya kazi kupitia timu za nchi na wataalam waliowekwa kwenye maeneo ya tukio kusaidia mamlaka za kitaifa kuimarisha maeneo muhimu ya kuchukua hatua, ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa magonjwa, upimaji wa ugonjwa na huduma za matibabu, kinga ya maambukizi na kudhibiti.
WHO inafanya kazi na mamlaka za afya kupata tiba, kuimarisha huduma za maabara kwa uwezo bora wa uchunguzi, na kuongeza juhudi za uelewa kuhusu hatari ya ugonjwa huu katika jamii.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, ameita kikao cha dharura cha kamati ya wataalam ili kubaini endapo mlipuko huu ni tishio la afya la umma la Kimataifa.
Dkt. Moeti amesema kuwa Shirika la WHO linafanya kazi kwa karibu na nchi kutengeneza mikakati na mipango yao ya chanjo, ili kuanzisha chanjo mara tu zitakapopatikana kwani chanjo ni moja ya zana nyingi za afya ya umma zinazotumika kudhibiti mpox.
Kwa kutamatisha Dkt. Moeti ameonya kuwa matibabu ya wagonjwa wa mpox ni yanategemea dalili za mgonjwa. Hata hivyo aesema tiba mbalimbali zinaweza kuwa na ufanisi dhidi ya mpox na kwamba kinga na udhibiti vinategemea kuongeza uelewa katika jamii na kuelimisha wahudumu wa afya ili kuzuia maambukizi na kukomesha usambaaji wake.
♦ SOMA ZAIDI hapa Kuhusu Ugonjwa huu wa homa ya nyani, au Mpox
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!