TAASISI ya Tiba ya Mifupa, Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza, imefanya upasuaji wa nyonga na magoti kwa wagonjwa 20, wakiwamo nane wa marudio.
Wakati hayo yakifanyika, taasisi hiyo imesema kuna ongezeko la tatizo na mahitaji ya upasuaji huo nchini na kwamba hadi sasa wagonjwa 12,000 wameshapatiwa huduma hiyo upasuaji na wengi wanaougua ni kuanzia miaka 50 na kuendelea.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk. Lemeri Mchome, aliyasema hayo jijini Dar es Salaam, wakati taasisi hiyo ikiadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake ikiweka kambi ya siku nne iliyoanza jana, kwa kuwafanyia upasuaji huo wagonjwa hao.
Alisema kambi hiyo inafanywa na MOI kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka Oxford na wengine kutoka Australia, ili kufanikisha upasuaji huo.
Kuhusu miaka 20 ya taasisi hiyo, Dk. Mchome alisema wagonjwa wengi ambao wanafanya upasuaji wa kurudia, wengi wao wana matatizo katika mifupa kwa kuwa na uvimbe unaohitaji huduma ya aina hiyo, ambao awali walitibiwa nje ya nchi.
“Tuna uwezo wa vifaa na miundombinu kwa kufanya upasuaji huu. Hii ni kutokan ana uwekezaji wa serikali. Tangu tumeanza kufanya upasuaji ni wagonjwa zaidi ya 5,000 ambao tumewatibu kwa kuwabadilishia nyonga na magoti.
“Upasuaji wa magoti pekee ni wagonjwa wengi zaidi wapatao 8,000 wana matatizo mbalimbali ambayo hayahitaji kubadilishwa lakini wanahitaji tiba mbadala,” alisema Dk. Mchome.
Aliongeza kwamba tatizo ni kubwa na kwa uzoefu katika takwimu zinaonesha bado kuna wagonjwa wengi wa kubadilisha nyonga na magoti takribani 200 wanaosubiri huduma.
“Arusha pekee katika kambi, tulipata wagonjwa 104 ambao tayari wanasubiria upasuaji wa nyonga na magoti. Bado tuna zaidi ya wagonjwa 50 katika foleni ya kusubiri upasuaji wa kurudia wa nyonga na magoti,” alibainisha Dk. Mchome.
Bingwa Mbobezi katika Upasuaji wa Mifupa na Uti wa Mgongo na Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa Mifupa MOI, Dk. Anthony Assey, alisema kwa miaka 20 taasisi hiyo inafurahia mafanikio ya upasuaji wa aina hiyo ambao ni wa kibingwa.
Alisema pia huduma kama hiyo, imefikishwa na taasisi hiyo katika hopitali tofauti nchini ikiwamo Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Bugando, Hospitali ya Tiafa Muhimbili (MNH)-Mloganzila na Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) na Mnazi Mmoja ya Zanzibar na zingine za kanda.
“Miaka 20 hii ni ya kazi kubwa na kambi inayoanza leo (jana) kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Oxford kutoka Uingereza kwa ufadhili wa kampuni ya Signature kutoka Australia, tunatarajia kufanya upasuaji wa marudio kwa wagonjwa wanane na wengine 12 upasuaji wa mara ya kwanza.
“Matatzio haya ya magoti ni ambayo yapo sana na takwimu inaonesha, watu waliofikisha zaidi ya miaka 50 matatizo huanza na unapofikisha umri wa zaidi ya miaka 60 kwa asilimia 50 watakuwa na maumivu ya aina fulani ya magoti na nyonga.
“Na umri unapokwenda zaidi ndipo upasuaji unapohitajika, na ukishafanyiwa unahitajika kufanyiwa marudio baada ya miaka 15, ili kubadilisha kifaa baada ya kuwa katika uchakavu,” alisema.
Naye Bingwa Mbobezi wa Nyonga na Misuli kutoka Houston, Texas nchini Marekani, Dk. William Stocks, alisema kupitia taaisi anayofanyia kazi, alibaini kwa nchi zinazoendelea ni kikwazo kwa watu wake kupata huduma aina hiyo, kutokana na gharama za upasuaji zinazofikia zaidi ya dola 2,000 za kimarekani.
“Taasisi yetu ikaamua kushirikiana na MOI kutoa huduma hiyo kwa nchi za eneo hilo, ikiwa ni mpango wa kiutu, tunatarajia kufanya huduma hiyo kwa Watanzania wengi ambao wana tatizo,” alisema Dk. Stocks.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!