Kuongezewa Njia Wakati Wa Kujifungua,jinsi hufanyika pamoja na sababu Zake
Kuongezewa Njia Wakati Wa Kujifungua,jinsi hufanyika pamoja na sababu Zake
Fahamu Kuongezewa njia kwa mama mjamzito wakati wa kujifungua kwa kitaalam Episiotomy ni kitendo kinachohusisha kuchana ngozi iliyopo kati ya uke na sehemu ya haja kubwa,
Kitendo hiki hufanyika wakati wa kujifungua lengo likiwa kupanua uke wa mama anayejifungua ili mtoto anayezaliwa apite kwa urahisi.
Jinsi kuongezewa njia wakati wa kujifungua hufanyika
Wakati mtoto anazaliwa na wataalam wa afya wameona kuna haja ya mama kuongezewa njia, mkunga au daktari hutia dawa ya ganzi na kisha hukata mara moja au mara mbili,
Mkato huu huweza kuwa wa mlalo (kutoka kulia kwenda kushoto au kushoto kwenda kulia). Aina nyingine ya mkato, hufanyika moja kwa moja kutoka kwenye uke kuelekea kwenye Njia ya haja kubwa.
Mikato yote hii hufanya uke kuongezeka upana. Baada ya mtoto na kondo la nyuma kuzaliwa, mkato huu hushonwa vyema kwa nyuzi maalumu.
Wakina mama wanaohitaji kuongezewa njia wakati wa kujifungua
Fahamu huko nyuma Swala la mama mjamzito kuongezewa njia wakati wa kujifungua lilikuwa la kawaida, na utaratibu huu ulikusudiwa kupunguza uwezekano wa kuchanika kwa uke wakati wa kujifungua. Siku hizi, haishauriwi kufanya utaratibu huu bila sababu ya msingi.
- Kuongezewa njia hufanyika kunapokuwepo ugumu wakati wa kujifungua.
- Kuongeza njia wakati wa kujifungua kunaweza kukahitajika wakati kichwa au mabega ya mtoto yanapokua makubwa kuliko uke wa mama,
- au kama mtoto amekaa vibaya (kama ametanguliza miguu au matako) wakati wa kujifungua na kusababisha matatizo wakati wa kujifungua.
- Inaweza pia kuhitajika ili kuharakisha mchakato wa kujifungua kama kuna wasiwasi kuhusu mapigo ya moyo ya mtoto.n.k
Nini cha kutarajia baada ya kuongezewa njia wakati wa kujifungua?
Mkato unaotokana na kuongezewa njia hupona bila matatizo na inaweza kuwa rahisi kutibu mkato wa aina hii kuliko mchaniko unaotokea wenyewe wakati wa kujifungua.
Unaweza kuendelea na shughuli zako za kawaida muda mfupi tu baada ya kujifungua. Nyuzi zinazotumika ni maalumu na hazihitaji kutolewa baadae. Unaweza kupunguza maumivu kwa kutumia dawa za kutuliza maumivu kwa masaa 24 ya kwanza.
Matatizo yanayoweza kutokea wakati au baada ya kuongezewa njia
Tafiti nyingi zimegundua kuwa utaratibu huu hauna faida yoyote ukifanyika kwa uzazi usiokuwa na matatizo yoyote. Na hakuna ushahidi unaoonyesha kwamba utaratibu huu unaboresha tendo la ndoa kwa mwanamke kama baadhi ya nadharia za watu,
Pia imegundulika kuwa baadhi ya wanawake walioongezewa njia wakati wa kujifungua huweza kupata maumivu wakati wa kujamiiana na huchukua muda mrefu kidogo kuanza kufanya tendo tena baada ya kujifungua.
Endapo mkato huu umeongezeka mpaka kuifikia misuli inayozunguka Njia ya haja kubwa inaweza kusababisha matatizo baadaye, mgonjwa anaweza kushindwa kuzuia gesi(kujamba) au kinyesi n.k
Hatari nyingine ni pamoja na:
- Kuvuja damu
- Kushindwa kuzuia kinyesi au gesi
- Maambukizi ya magonjwa
- Kuvimba n.k
Endapo kuna hali yoyote kwenye eneo la mshono au mkato ambayo huielewi hakikisha unawasiliana na wataalam wa afya kwa Msaada zaidi.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!