Mlipuko mpya wa kipindupindu waleta taharuki kwa wakimbizi Sudan

Mlipuko mpya wa kipindupindu waleta taharuki kwa wakimbizi Sudan

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR kupitia mwakilishi wake nchini Sudan Kristine Hambrouck, katika mkutano na waandishi wa habari leo huko Geneva, limesema wimbi jipya la kipindupindu nchini Sudan, ambalo ni mlipuko wa pili tangu kuanza kwa vita miezi kumi na sita iliyopita, linatishia jamii zilizohamishwa nchini kote.

Kristine Hambrouck akiwa Port Sudan amewaeleza waandishi waliokuwa Geneva, Uswisi kwamba idadi ya jumla ya maambukizi ya kipindupindu ya wakimbizi yanasemwa kuwa ni 119 katika maeneo matatu ya wakimbizi jimboni Kassala, kama ilivyoripotiwa na Wizara ya Afya ya Sudan, huku wakimbizi watano wamefariki baada ya kuugua ugonjwa huo.

Mbali na kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu, ongezeko la maambukizi ya magonjwa yatokanayo na maji yakiwemo malaria na kuhara, pia vinaripotiwa. Vikwazo katika ufikiaji wa kibinadamu pia vinaathiri juhudi za kukabiliana. Mapigano, ukosefu wa usalama na mvua zinazoendelea kunyesha vinatatiza usafirishaji wa misaada ya kibinadamu. Katika majimbo ya Sennar, Blue Nile, Jazirah, White Nile, Darfur, na Kordofan – nyumbani kwa zaidi ya wakimbizi milioni 7.4 na wakimbizi wa ndani wa Sudan – changamoto za upatikanaji zimechelewesha utoaji wa dawa muhimu na vifaa vya msaada.

Juhudi zinaendelea kufanyika

Licha ya changamoto hizo zinazokabili ufikishaji wa misaada nchini Sudan, Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani WHO linaendelea kushirikiana na UNHCR kutoa misaada ya chanjo ambapo watu 94,000 watapewa chanjo katika kambi ya Minkaman, Kaunti ya Awerial, ikilenga watu waliokimbia makazi yao na jamii zinazowapokea, ikifuatiwa na kampeni za chanjo katika kambi zilizoko Juba, zinazojumuisha zaidi ya watu 43,000.

“Kambi ya Minkaman katika Kaunti ya Awerial na kambi ya Juba imechaguliwa kwa sababu ya uthabiti wa hali na ufikiaji rahisi katika maeneo hayo,” anasema Dk Abdinasir Abubakar, kutoka timu ya WHO ya Ufuatiliaji na Mwitikio wa Magonjwa, nchini Sudan Kusini.

Dk Abdinasir anaongeza kuwa “Pia tunaangalia kambi zingine, na mara ufikivu na usalama utakapoimarika, tutapanua kampeni za chanjo ya kipindupindu katika maeneo haya. Tutakuwa tukipitia hali hiyo siku baada ya siku.”

Tangu kuanza kwa mzozo nchini Sudan, zaidi ya  watu milioni 10.3 wamefukuzwa kutoka makwao na kujihifadhi mahali pengine ndani ya Sudan au katika nchi jirani. Huku hali ya kibinadamu na kiwango cha ufadhili tayari kikiwa hatarini kabla ya mlipuko huu wa hivi punde wa kipindupindu, fedha zinahitajika sana kusaidia utoaji wa huduma za afya na misaada mingine ya kuokoa maisha ikiwa ni pamoja na upanuzi wa vituo vya matibabu ya kipindupindu na vituo vingine vya afya, wafanyakazi wa ziada wa afya, na kuongezeka kwa akiba ya maji na dawa.

Kwa nini chanjo inahitajika dhidi ya kipindupindu?

Mosi, Kipindupindu ni ugonjwa wa kuhara unaosababishwa na kumeza chakula au maji machafu na huathiri watoto na watu wazima. Inaweza kuua kwa muda mfupi sana kutokana na upungufu wa maji mwilini.

Pili, Watoto wako kwenye hatari kubwa ya kuambukizwa. Mara baada ya kuambukizwa, pamoja na upungufu wa maji mwilini, watoto hupata hypoglycemia kali ambayo inaweza kusababisha coma na kifo. Vile vile, makundi ‘yalio katika hatari’ (kwa mfano watu wenye utapiamlo, wazee, wanawake wajawazito, watu walio na magonjwa sugu makali, wagonjwa wa UKIMWI) wana uwezekano mkubwa wa kupata aina kali za ugonjwa huo.

Tatu, Chanjo ya kipindupindu ni zana salama na madhubuti ya ziada ambayo inaweza kutumika chini ya hali sahihi ili kuongeza hatua zilizopo za udhibiti wa kipindupindu.

Kati ya dola bilioni 1.5 zinazohitajika na UNHCR na washirika wengine kwa Mpango wa Kikanda wa Kukabiliana na Wakimbizi (RRRP) ili kutoa msaada katika nchi zinazopakana na Sudan lakini had isas ni asilimia 22 tu ndiyo imepokelewa.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!