Mpox yaingia Sweden, WHO yataka mshikamano kudhibiti
Homa ya nyani au mpox aina ya Clade 1B imevuka barani Afrika na kuingia Ulaya hususan Sweden, ikiwa ni nchi ya kwanza nje ya bara hilo kuthibitisha kuwa na ugonjwa huo ambao tayari WHO imetangaza kuwa ni dharura ya afya ya umma duniani.
Taarifa hizo ni kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, WHO kanda ya Ulaya.
Juzi Jumatano WHO ilitangaza kuwa mpox ni dharura ya afya umma duniani baada ya kasi kubwa ya kusambaa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kwa Clade 1B ambavyo ni virusi vipya vya mpox na hatari zaidi, ikilinganishwa na vile vya awali vya mwaka 2022.
Hans Klugeambaye ni Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Ulaya, amenukuu mamlaka za afya nchini Sweden zikisema kuwa mgonjwa huyo alisafiri maeneo ya Afrika yanayokabiliwa na mlipuko wa mpox, ingawa hakutaja eneo husika.
Kluge amesema walishaeleza awali kuwa haitochukua muda mrefu kwa virusi hivyo vipya vya mpox kusambaa maeneo mengine nje ya Afrika kwa kuzingatia muunganiko wa dunia.
Kwa sasa mgonjwa anatibiwa dalili za ugonjwa huo, sambamba na kumtenga na kufuatilia waambata wake.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus kupitia ukurasa wake wa X zamani Twitter, amesema kubainika kwa mgonjwa Sweden kunasisitiza umuhimu wa nchi zenye maambukizi kushirikiana kukabili virusi hivyo.
Ametaka nchi ziimarishe ufuatiliaji, zibadilishane takwimu na kufanya kazi pamoja kuelewa njia za maambukizi, kushirikishana chanjo na kujifunza kutokana na masomo ya awali wakati mpox ilipotangazwa kuwa dharura ya afya ya umma duniani.
Barani Afrika, mlipuko wa mpox umethibitishwa DRC na Burundi, huku Kenya, Uganda na Côte d’Ivoire zikiwa na wagonjwa tu wa hapa na pale.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!