Ulaji hafifu shuleni utachangia watoto kukosa akili ya maisha

Profesa wa Lishe kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA), Joyce Kinabo amesema ulaji hafifu shuleni utachangia watoto kukosa akili ya maisha na kujikwamua kutoka katika umaskini pale watakapokuwa wakubwa.

Amesema lishe bora ina umuhimu mkubwa kwa watoto ambao wanatakiwa kuja kuhimili maisha wanayoyaendea, hivyo wanapaswa kulishwa vyakula mchanganyiko. Amesema watoto wanapata mabadiliko ya kimwili na wanapaswa kupata virutubisho.

“Kama Taifa likishindwa kulisha ubongo wa watoto, basi tujihesabu tumeshindwa. Tuhakikishe watoto wetu wanapata vyakula vitakavyowakuza vizuri na wawe na akili zakutosha. Mabadiliko ya kimwili ndio yanayoendeleza mahitaji ya lishe na inapatikana katika vyakula mbalimbali, kwa wastani mwili wa binadamu unahitaji virutubisho zaidi ya 40 kwa siku vinavyopatikana katika vyakula mbalimbali,” amesema.

Amebainisha hayo siku ya Jumatatu Agosti 12, 2024 wakati akichangia mjadala kwenye Mwananchi X Space, inayoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa kushirikiana na Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) Tanzania pamoja na Taasisi ya Lishe na Chakula Tanzania (TFNC) wenye mada isemayo ‘Umuhimu wa kuwapa chakula mchanganyiko watoto wa shule.’

Amesema ndio maana kuna mbogamboga, matunda, nyama, dagaa, marahage na jamii ya mikunde na vinashirikiana katika matumizi yake mwilini.

Aidha, ameshauri vyakula vinavyouzwa nje ya nchi vinatakiwa kuwalisha watoto wetu, ili wapate akili na ufanisi.
“Uwezo wa kuwalisha vyakula tunao, tunachotakiwa ni kujipanga kama Taifa na njia zipo nyingi kuanzia kuhamishisha wazazi wajue faida za kuwalisha watoto vyakula mchanganyoko, basi kila mtu atakuwa tayari kuchukua nafasi yake ili kuchangia ubora wa vyakula shuleni pamoja na mazingira,” ameshauri Profesa Kinabo.

(Imeandikwa na Sute Kamwelwe)
#mwananchiupdates
#tunaliwezeshataifa

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!