Unyonyeshaji usio wa kutosha husababisha asilimia 16% ya vifo vya watoto kila mwaka
Takwimu za hivi karibuni za shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, zinakadiria kuwa unyonyeshaji usio wa kutosha husababisha asilimia 16 ya vifo vya watoto kila mwaka.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linahimiza akina mama kuungwa mkono na jamii, familia, na wahudumu wa afya wakati wa kunyonyesha.
Kwa kuunda mifumo rafiki ya unyonyeshaji, na kuheshimu haki ya wanawake ya kunyonyesha wakati wowote, mahali popote, na kukuza usaidizi wa kijamii.
Wiki ya Kunyonyesha Duniani hufanyika katika wiki ya kwanza ya Agosti kila mwaka. Kauli Mbiu ya 2024 ni ‘Kuziba pengo: Usaidizi wa Kunyonyesha kwa wote.’
Lakini bado kuna imani potofu kuhusu kunyonyesha, ambazo zinaweza kuwazuia wanawake kunyonyesha. Tumewauliza wataalamu wawili kuzisawazisha imani hizi.
Catriona Waitt ni profesa wa dawa za binaadamu na afya ya umma, katika Chuo Kikuu cha Liverpool na mtafiti katika Chuo Kikuu cha Makerere, Kampala, Uganda katika kitengo Health Science.
Mwingine ni Alastair Sutcliffe, profesa wa magonjwa ya watoto kutoka Chuo Kikuu cha London, Uingereza.
Titi kuuma sio jambo la kawaida
Prof Waitt: Kwa siku za awali ni kawaida ziwa kuuma kabla hujazoea. Lakini kunyonyesha hakupaswi kuumiza au kusababisha maumivu makali.
Kuuma kwa chuchu inaweza kuwa ni dalili ya maambukizi au mtoto hanyonyi itakiwavyo. Maumivu madogo ya awali ni kawaida, haswa kwa akina mama wanaoanza kuzoea kunyonyesha.
Subiria kabla ya kunyonyesha
Prof Sutcliffe: Jambo lolote linalohimiza akina mama kunyonyesha ni zuri kwa afya ya binadamu. Hakuna ushahidi wa kisayansi kwamba mama anapaswa kuvuta muda kabla ya kuanza kunyonyesha baada ya kujifungua.
Kizuizi chochote cha kunyonyesha baada ya kujifungua hakina mashiko ya kisayansi. Na kuna faida nyingi za mtoto kunyonya mara tu baada ya kujifungu.
Kunyonyesha ni lishe kwa mtoto. Pia husaidia kusinyaa kwa mfuko wa uzazi, na kusaidia kuzuia au kupunguza kasi ya kutoka damu baada ya kujifungua.
Pia, katika siku chache za kwanza baada ya kujifungua, mwili wa binadamu hutoa protini maalumu inayoitwa kolostramu, ambayo hufanya maziwa kuzalishwa.
Huwezi kutumia dawa yoyote ikiwa unanyonyesha
Prof Waitt: Hilo huwa ni swali la kwanza kwa mama popote duniani. Je, dawa yoyote ni salama kwa mtoto wangu?
Ukweli ni kwamba dawa nyingi humfikia mtoto katika kiwango cha chini sana. Ikiwa daktari anasema unahitaji dawa, uliza maswali yako lakini kuna uwezekano mkubwa kuwa dawa hiyo ni salama kutumia.
Kile ambacho mtoto anahitaji zaidi ya yote ni mama mwenye afya. Dawa nyingi zinazoshughulikia maambukizi, uchovu au maumivu zinaweza huwa ni salama.
Na dawa ambazo hazipaswi kutumiwa wakati wa kunyonyesha, ni chache sana. Mara nyingi ni kwa ajili ya matibabu ya hali mbaya sana za afya kama vile saratani.
Kuna dawa nyingine ambazo tumia kwa uangalifu kwa kuzingatia hatari na faida. Mwanamke yeyote ambaye anapewa dawa wakati wa kunyonyesha anapaswa kumuuliza daktari maswali.
Mfano dawa za mafua, kupiga chafya au koo kuwasha, ambazo zinafungua mishipa – hizi zinaweza kupunguza mtiririko wa maziwa.
Na kuwa mwangalifu na dawa za mitishamba kwa sababu huwezi kujua zina nini ndani yake, na nyingi ya dawa hizo hazijafanyiwa utafiti wa kina.
Epuka chakula chenye viungo
Prof Waitt: Hakuna kitu ambacho mama hapaswi kula anaponyonyesha. Lakini maziwa ya mama yanaweza kuathiriwa na ulaji wako.
Kwa mfano, niligundua nikinywa juisi ya matunda ya jamii ya machungwa, mtoto wangu huwa na hasira sana.
Wakati mwingine unaweza kugundua tabia za mtoto wako kwa chakula ambacho umekula. Lakini hakuna kitu ambacho kinamdhuru au sio sahihi kiafya na ambacho kinahitaji kuepukwa.
Usitumie maziwa ya unga kama unanyonyesha
Prof Waitt: Mwili wa mwanamke umeumbwa kuwa na uwezo wa kutoa maziwa ya kutosha kwa mtoto wako. Mtoto anaponyonya chuchu, huchochea homoni kutoa kiasi kinachohitajika cha maziwa.
Kwa hivyo, ikiwa unanyonyesha mtoto mdogo, mkubwa au hata mapacha, mwili wako utatoa maziwa ya kutosha.
Ukianza kumpa maziwa ya unga, homoni zitajizuia. Mwili wako hautopata ishara za kutosha kwamba mtoto anahitaji maziwa zaidi.
Ikiwa unakabiliwa na tatizo la uhaba wa maziwa na ukaanza kumpa mtoto maziwa ya kopo, hilo linaweza kukupa nafuu ya muda mfupi, lakini tatizo la uhaba wa maziwa linaweza kuwa kubwa.
Kwa upande mwingine, ikiwa umechoka usiku au ni mgonjwa na mpenzi wako anampa mtoto maziwa ya unga ili apumzike, hiyo haimaanishi huwezi kunyonyesha. Kwa hivyo maziwa ya unga sio jambo baya, lakini yanaweza yasiwe na msaada mzuri.
Usinyonyeshe ukiwa mgonjwa
Prof Sutcliffe: Hapana, hiyo ni imani potofu. Hali pekee ambayo mtu hapaswi kunyonyesha ni ikiwa ana VVU au homa ya manjano. Virusi hivyo vinaweza kupita kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Akina mama wanapokuwa wagonjwa miili yao hutoa kingamwili ambazo pia hulinda watoto wao wachanga. Ni nadra sana kuona ugonjwa wa mama anaenyonyesha ukimpata mtoto.
Vigumu kumwachisha mtoto baada ya mwaka
Prof Waitt: Shirika la Afya Ulimwenguni linapendekeza kwamba unapaswa kunyonyesha maziwa ya mama pekee kwa miezi sita, na kisha kumwanzishia lishe ya ziada lakini uendelee kumnyonyesha kwa muda unaotaka. Hakuna wakati uliopendekezwa wa kuachisha.
Katika baadhi ya nchi zenye kipato cha juu kama vile Uingereza, watoto wengi huachishwa wakiwa na mwaka mmoja hadi miwili.
Katika nchi nyingine zenye kipato cha chini, kama vile Uganda, unyonyeshaji huendelea hadi mtoto anafika miaka miwili ama mitatu.
Tatizo ni kwamba nchi nyingi hazina likizo ya kutosha ya uzazi inayoruhusu akina mama kunyonyesha maziwa mama pekee kwa mujibu wa WHO.
Via:Bbc
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!