Ushauri watolewa ili kuimarisha kinga dhidi ya Ugonjwa wa Mpox,Homa ya Nyani

Ushauri watolewa ili kuimarisha kinga dhidi ya Ugonjwa wa Mpox,Homa ya Nyani

WADAU wa afya wameshauri jamii kuendelea kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa homa ya nyani kwa kula vyakula vyenye kuongeza kinga ya mwili na kuepuka kugusana.

Ushauri huo umekuja ikiwa ni takribani wiki mbili tangu serikali itahadharishe wananchi kuhusu ugonjwa huo ulioripotiwa katika nchi jirani za Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Ofisa Mawasiliano ya Afya Wakati wa Dharura Wizara ya Afya – Idara ya Kinga, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, Oscar Kapera, alisema mwishoni mwa wiki kuwa licha ya kuwa ugonjwa huo haujaingia nchini, ni muhimu wananchi, hasa wanaoishi mipakani kuchukua tahadhari.

Alisema ugonjwa wa homa ya nyani husababishwa na virusi vinavyojulikana kama ‘monkey pox’ na huambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu au kutoka kwa mtu mmoja kwenda mwingine kwa kugusana na mtu mwenye dalili za ugonjwa.

Alitaja dalili kuu ya mtu mwenye ugonjwa wa mpox ni kuwa na vipele maeneo mbalimbali ya mwili, ikiwamo uso, mikono, miguu na sehemu za siri.

“Vipele hivi hufanana na vipele vingine ila huweza kutofautishwa kwa kuwa vinaambatana na kuvimba, homa, maumivu ya kichwa, vidonda kooni, maumivu ya viungo vya mwili ikiwamo misuli na mgongo,” alisema.

Aliongeza kuwa mtu yoyote anaweza kupata ugonjwa; wale ambao kinga ya mwili ipo chini wapo kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa huo.

Daktari Bingwa wa Tiba ya Familia kutoka Hospitali ya Agakhan, Willbroad Kyejo, alisema ugonjwa huo unaweza kuzuiliwa na usisambae nchini kama hatua stahiki zitachukuliwa na kila mmoja kutimiza wajibu wa kujikinga.

Alishauri kila mmoja kuzingatia kanuni za afya, elimu ya afya na maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya, huku akitaja mambo ya kuzingatia kuwa ni pamoja kuepuka kugusana na mtu anayeonesha dalili za ugonjwa huo.

Alishauri pia kuepuka kugusa wanyama wa porini, hasa wale wanaoonesha dalili za ugonjwa na kuhakikisha nyama ya porini inapikwa vizuri kabla ya kuliwa.

Alishauri wanaohudumia wagonjwa  mwenye dalili za homa ya nyani, kama vile vipele na vidonda, wahakikishe wanavaa vifaa vya kujikinga kama barakoa na glavu.

“Pia epuka kugusa ngozi ya mtu mwenye dalili hizi bila kinga sahihi,” alisema na kushauri wale waliopo katika hatari ya kupata ugonjwa huo kupatiwa chanjo.

Alisisitiza pia ni muhimu kunawa mikono mara kwa mara kwa sabuni na maji safi na yanayoririka, kutumia vitakasa mikono pamoja na kuepuka kugusa majimaji ya mwili, ikiwamo damu, vipele, mate na manii ya mtu mwenye dalili za ugonjwa huo.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, pamoja na mawaziri wa afya wa nchi za Afrika wanatarajiwa kukutana kwa dharura kabla ya mwisho wa mwezi huu kujadiliana na kupitisha mikakati ya pamoja na kuchukua hatua za haraka kukabiliana na ugonjwa huo.

#SOMA ZAIDI hapa Kuhusu Ugonjwa huu wa Mpox au homa ya nyani,Chanzo, dalili na Tiba

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!