Ticker

6/recent/ticker-posts

kampeni ya utoaji chanjo kwa watoto yaanza huko Gaza



kampeni ya utoaji chanjo kwa watoto yaanza huko Gaza

WHO

Kampeni ya Umoja wa Mataifa ya chanjo ya polio inaendelea katikati mwa Gaza

Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina UNRWA Phillipe Lazzarini amesema awamu ya kwanza ya zoezi kubwa la kampeni ya utoaji chanjo ya polio kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka 10 limeanza rasmi hii leo huko katikati mwa ukanda wa Gaza, huku akieleza kuwa kampeni hii inakimbizana na muda ili iweze kufikia watoto 600,000 katika ukanda huo.

Katika taarifa yake aliyoichapishwa kwenye mtandao wa X hii leo Lazzarini amesema mama mmoja amemueleza anahisi ahueni baada ya mtoto wake kupata matone mawili ya dozi ya chanjo ya polio katika kliniki ya UNRWA.

Hata hivyo kiongozi huyo wa UNRWA amesisitiza kuwa ili kampeni hiyo iweze kufanikiwa, pande zote katika mzozo unaoendelea huko Gaza ni lazima ziheshimu sitisho la muda la mapigano katika ukanda huo.

“Kwa ajili ya watoto wa ukanda huu, ni wakati wa kuwa na sitisho la kudumu la mapigano,” aliongeza Lazzarini.

Kwa upande wake, Sam Rose, Kaimu Mkurugenzi wa Operesheni za UNRWA huko Gaza, kupitia chapisho kwenye mtandao wa X ameeleza kwamba, timu za mawakala zitawafikia maelfu ya watoto na kuwapatia chanjo ya polio katika kliniki, vituo vya afya na kupita kutoka hema hadi hema katika Ukanda mzima.

Amesisitiza kuwa UNRWA itatoa chanjo hadi kwa nusu ya watoto hao, na takriban wafanyakazi 1,100 wa shirika hilo watashiriki katika kampeni hiyo inayofanywa na Wizara ya Afya ya Palestina kwa ushirikiano na UNRWA, WHO na UNICEF.

Chanjo bora zaidi ni amani

Akizungumzia kuhusu kuanza kwa zoezi hilo la utoaji chanjo kwa watoto walioko Gaza, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema watoto hao wa Gaza wanapokea chanjo hiyo inayohitajika zaidi.

Hata hivyo Dkt.Tedros amesema suluhisho la kweli ni amani “Mwisho wa wote, chanjo bora zaidi kwa watoto hawa ni amani”

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kanda wa Shirika la Afya Duniani kwa Mashariki ya Mediterania, Dkt. Hanan Balkhi, amesema kuwa kuna haja ya chanjo hiyo kufikia angalau asilimia 90 ya wanaotarajiwa kupatiwa.

“Shukrani nyingi kwa pande zote zinazohakikisha usalama wa wafanyakazi wa afya, watoto na familia katika nyakati hizi ngumu”.

Nalo shirika la Umoja wa Mataiafa linaloshughulikia masuala ya watoto UNICEF limesisitiza kuwa pande zote lazima ziheshimu vipindi vya sitisho la mapigano kwa sababu za kibinadamu lililo bainishwa kwa kila eneo wakati wa kampeni hiyo ya utoaji chanjo.



Post a Comment

0 Comments