Njia ya Vipandikizi yatumika zaidi miongoni mwa wanawake

Njia ya Vipandikizi yatumika zaidi miongoni mwa wanawake.

Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania (TDHS) ya mwaka 2022 unaonyesha asilimia 45 ya wanawake wenye uwezo wa kufanya tendo la ndoa wanaotumia njia za uzazi wa mpango, asilimia 36 wanatumia njia za kisasa na asilimia nane wanatumia za asili.

Hata hivyo, njia ya vipandikizi ndiyo inayotajwa kutumika zaidi miongoni mwa wanawake kwa asilimia 14 ikifuatiwa na njia ya sindano kwa asilimia tisa.

Hayo yamebainishwa na Mhariri wa Afya wa Mwananchi, Herieth Makwetta Siku ya Jumatano, Septemba 25, 2024 wakati akichokoza mada kwenye mjadala wa Mwananchi Space, ulioandaliwa na Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa kushirikiana na Marie Stopes Tanzania @mariestopestz isemayo ‘Uhuru wa Kuamua: Namna upatikanaji wa haki muhimu za afya ya uzazi unavyochangia maendeleo Tanzania’. 

Amesema takwimu zinaonyesha mwaka 2022 vifo vitokanavyo na uzazi vilikuwa 104 kwa kila vizazi hai 100,000. Hata hivyo, lengo la Serikali ni kupunguza vifo kutoka 104 katika kila vizazi hai 100,000 hadi 70 kufikia mwaka 2025.

“Uzazi wa mpango ni muhimu kwa maendeleo ya Tanzania, kwani huokoa maisha kwa kusaidia kupunguza magonjwa ya kina mama na vifo, na kuongeza viwango vya kuishi kwa watoto wachanga,” amesema. 

Amefafanua kuwa uzazi wa mpango ni sehemu ya kuboresha afya ya mama na mtoto lakini pia kujenga uchumi wa familia na Taifa kwa ujumla. 

Amesema kwamba upatikanaji wa uzazi wa mpango wa hiari na huduma ya afya ya uzazi kwa wanandoa na watu binafsi ni muhimu katika kuhakikisha uzazi salama, familia zenye afya na jamii zinazostawi.

(Imeandikwa na Sute Kamwelwe)

Via; mwananchiupdates

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!