UNICEF yatangaza zabuni ya dharura ya chanjo za mpox
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhumia watoto UNICEF limetangaza zabuni ya dharura kwa ajili ya Kununua chanjo za ugonjwa wa homa ya nyani au mpox. Chanjo ambazo zinaaminika kuwa na jukumu muhimu katika kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa mpox ambao umetangazwa kuwa dharura ya afya ya umma na shirika la afya ulimwenguni WHO pamoja na kituo cha kudhibiti na kuzuia magonjwa barani afrika CDC.
Zabuni hii ya dharura imetolewa rasmi ili kuhakikisha chanjo zinazopatikana kwa haraka na pia kupanua uzalishaji. Makubaliano ya uzalishaji wa hadi dozi milioni 12 ifikapo mwaka 2025 yanaweza kufikiwa hii itategemea mahitaji na uwezo wa uzalishaji wa watengenezaji pamoja na ufadhili.
Katika zabuni hii ya dharura, UNICEF itaweka mikataba itakayo ainisha masharti ya ugavi kwa watengenezaji wa chanjo. Hatua hii itawezesha UNICEF kununua na kusafirisha chanjo bila kuchelewa mara tu nchi na wadau watakapokuwa wamepata ufadhili, wamethibitisha mahitaji na utayari, na mahitaji ya udhibiti wa kukubali chanjo yamewekwa.
Akizungumzia kuhusu umuhimu wa chanjo hizo, mkurugenzi wa kitengo cha ugavi wa UNICEF, Leila Pakkala amesema “Kushughulikia uhaba wa sasa wa chanjo ya mpox na kupeleka chanjo kwa jamii zenye uhitaji kwasasa ni jambo muhimu sana. Pia kuna haja kubwa ya kuweka utaratibu wa ugawaji wa kimataifa na wa uwazi ili kuhakikisha kuna upatikanaji sawa wa chanjo ya mpox.”
Nchini jamhuri ya Kidemokrasia Kongo DRC ambako ndiko kitovu cha ugonjwa huu kuna zaidi ya washukiwa wa ugonjwa wa mpox 18,000 na tayari vifo 629 vimeripotiwa mwaka huu pekee. Vifo vinne kati ya vitano vinavyoripotiwa ni vya watoto.
Mkurugenzi Mkuu wa CDC Afrika Dkt. Jean Kaseya amesema wakati huu wanapokabiliana na mlipuko wa mpox unaoendelea, ununuzi na usambazaji wa chanjo kwa wakati ni muhimu katika kulinda idadi ya watu walio hatarini zaidi, haswa katika kanda zilizo athirika zaidi.
Dkt. Kaseya amesema ushirikiano ndio suala muhimu kwasasa “Zabuni hii ya dharura ni hatua muhimu katika juhudi zetu za pamoja za kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huu. Afrika CDC imejitolea kuhakikisha kuwa chanjo zinatolewa kwa haraka na kwa usawa katika bara zima, kwa ushirikiano na UNICEF, Gavi, WHO, na wadau wengine muhimu. Mwitikio wetu wa umoja ni muhimu ili kupunguza athari za dharura hii ya afya ya umma na kulinda afya na ustawi wa jamii zetu.”
Chanjo ni mojawapo ya zana kadhaa zinazotumiwa kukabiliana na maambukizi na kulinda watoto na jamii dhidi ya mpox. Afrika CDC, Gavi, UNICEF, WHO, na wadau wengine wanatanguliza uzuiaji na udhibiti wa maambukizi, na mawasiliano ya hatari ya ugonjwa huu na ushiriki wa jamii katika mapambano.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!