Uvimbe wa kilo Tano waondolewa mwilini kwa Mgonjwa
HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH), imefafanua saa nne za upasuaji mkubwa aliofanyiwa Karume Ally Kalume, kumuondoa kilo tano za uvimbe mwilini, ambaye tatizo lake limebainika ni la kuzaliwa nalo.
Kadhalika, Kalume ambaye alilazwa hospitalini hapo kwa takribani siku 23, anasubiri kufanyiwa upasuaji wa pili katika hospitali hiyo, sehemu ya mguuni ambako pia kuna uvimbe.
Kalume, mwili wake ulikuwa unaota uvimbe maeneo tofauti ya mwili wake na kumsababishia uzito, alifika hospitalini hapo Agosti 28 na kisha kufanyiwa uchunguzi na upasuaji kufanyika Agosti 30, mwaka huu.
Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji Rekebishi Idara ya Upasuaji MNH na Bingwa wa Upasuaji Rekebishi, Dk Laurean Rwanyuma, amesema hayo leo, jijini Dar es Salaam kwamba, Kalume amefanyiwa upasuaji huo kwa kuondolewa uvimbe, baada ya kupokelewa katika wodi ya Kibasila.
"Vipimo vilifanyika vya damu na x-ray ili kubaini ana tatizo gani, matibabu yake yalihitaji kufanyiwa upasuaji kuondoa uvimbe shingoni, begani na kifuani. Agosti 30, mwaka huu aliingia chumba cha upasuaji kufanyiwa upasuaji huo, iliochukua takribani saa nne na wataalamu walioshiriki ni wanne.
Baada ya hapo alipokelewa wodi ya Sewahaji, ambako kipo kitengo cha upasuaji Rekebishi. Ugonjwa huu sio wa kuambukiza ni wa kuzaliwa nao. Mara nyingi mtoto anapozaliwa ni vizuri kuungalia mwili wake, inaweza uvimbe uwe haujatokeza, lakini kuna alama ambazo ukizingalia uwaambie wataalamu wajue ni kitu gani," amesema Dk. Rwanyuma.
Amesema Kalume alianza kupata uvimbe huo akiwa na umri wa miaka 15 na kwamba atahitaji matibabu mengine, kwa sababu ana uvimbe mdogo maeneo tofauti, ikiwamo mguuni.
"Amekuwa na uvimbe mkubwa asingeweza kuondolewa kila kitu, kwa sababu upasuaji ulikuwa ni mkubwa. Atahudhuria kliniki kila baada ya wiki mbili, tutapanga upasuaji mwingine kumalizia uvimbe. Hatuondi kila kitu, ila mkubwa tumeuondoa,"
Kalume mwenye umri wa miaka 41, ni mkazi wa Mbagala Kilungule, mtaa wa Mwinyi, wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, ameishi na tatizo hilo kwa takribani miongo miwili.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!