Vyakula vya mama mjamzito anavyostahili kula

Vyakula vya mama mjamzito anavyostahili kula

Fahamu kuhusu Vyakula Bora Ambavyo Mama Mjamzito Anastahili Kula ili Yeye na Mtoto Wawe na Afya Bora, Soma zaidi hapa kwenye Makala hii;

Kwa ajili afya ya mama na mtoto ni muhimu sana mama mjamzito apate chakula bora kilicho na madini yote kama vitamini na protini,

Mama mjamzito anatakiwa apate gramu 100 za protini kila siku. Mama mwenye ujauzito anapaswa kula vizuri kwa ajili ya afya yake na ile ya mtoto aliye tumboni.

Ifuatayo ni orodha ya baadhi ya vyakula ambavyo anatakiwa apate mama mjamzito kila siku ya ujauzito wake ili kuwa na afya bora.

Vyakula vya mama mjamzito anavyostahili kula

Vyakula bora ambavyo mama mjamzito na mtoto wake wanastahili kula Ni pamoja na;

1. chakula Jamii ya Kunde;

Mbegu za Kunde ni sehemu muhimu ya chakula kwa mama mjamzito kwa sababu huwa na kiwango kikubwa cha protini.

Kwa watu wasiokula nyama au wana uwezo mdogo tu kujipatia nyama mbegu za jamii ya kunde zinatosheleza mahitaji ya protini.

Hivi ni vyakula vya mimea kama vile;

  • Soya,
  • Peas,
  • Karanga,
  • Alfa alfa,
  • Mikunde,
  • maharage.

2. Mayai;

Mayai mawili kwa siku husaidia kuupa mwili protini, vitamini A na madini ambayo itasaidia kuzuia kupatwa na maradhi ya magonjwa mbali mbali.

3. Maziwa na vyakula vya jamii ya maziwa;

Ni muhimu mama mjamzito kupata Glasi nne au zaidi za maziwa ya aina yoyote pamoja na/au vyakula vyenye jamii ya maziwa kama jibini, mtindi na siagi.

Maziwa ni muhimu kwani yana protini, calcium, vitamini na virutubisho vingi.

Virutubisho hivi Vitasaidia ukuaji wa mifupa na misuli, Ni muhimu kwa kuongeza damu, kusaidia usingizi na kusawazisha mapigo ya moyo.

4. Viazi tamu;

Viazi vitamu vina vitamini A ambayo husaidia ukuaji wa macho ya mtoto,ngozi na mifupa

5. Nyama;

Nyama ya nguruwe,kuku au ng'ombe huwa na protini nyingi sana na husaidia katika ukuaji wa mwili wa mtoto hasa kwa mama mjamzito wa miezi minne.

6. Nafaka na vyakula vya Wanga;

Vyakula hivi huupa mwili nguvu ya kufanya kazi na pia ukuaji wa mtoto tumboni.

Vyakula hivi ni kama vile;

  • mahindi,
  • mtama,
  • mihogo,
  • vyakula vya ngano kama mkate n.k.

7. Matunda kama Parachichi;

Parachichi Ni matunda ambayo yana mafuta mengi maarufu kama fatty acid. parachichi inasaidia katika ukuaji wa ubongo,ngozi nyororo na ukuaji wa misuli ya mtoto tumboni.

8. Mboga za majani;

Mboga za majani kama spinach, kabeji, mchicha na matembele. Mboga hizi zinafaa ziwe zenye rangi ya kijani iliyokolea kwa sababu hizi ndizo zenye virutubisho vya kutosha.

Mboga hizi zitampa mama na mtoto wake Vitamin A na B, pia virutubisho vitakavyosaidia mwili kupata protini ya kutosha, ukuaji wa mwili, na utengenezaji wa damu. Kutopata mboga za kutosha kunaweza sababisha mama kupata ugonjwa wa Anemia(Upungufu wa damu).

9. Mafuta ya samaki;

Mafuta ya samaki huwa na Omega fatty acids ambayo inasaidia ukuaji wa ubongo na macho ya mtoto.

10. Maji;

Maji ni muhimu kwa mwili kwa sababu inasaidia kwenye mmenyenyo na unyonywaji chakula na pia husaidia kuzuia choo kigumu, Maji pia huzuia uvimbe wa mwili na maambukizi ya mfumo wa mkojo(UTI)

VYAKULA VYA KUEPUKA MAMA MJAMZITO

Je Ni vyakula gani vya kuepuka kula wakati wa ujauzito?

Ili mtoto azaliwe akiwa na afya njema pamoja na akili timamu, akiwa tumboni lazima alishwe lishe bora na mlo sahihi. Mwenye jukumu la kutoa lishe bora na sahihi kwa kiumbe kilichomo tumboni ni mama. Anatakiwa kujua aina ya vyakula anavyopaswa kula. Vivyo hivyo, anatakiwa kujua aina ya vyakula vya kuviepuka.

Katika makala ya leo, tunaangalia Pia orodha ya vyakula vilivyokatazwa. Mama mja mzito haruhusiwi kuvila vyakula vifuatavyo kwa faida ya kiumbe kilichomo tumboni na kwa faida yake mwenyewe:

1. Nyama mbichi

Epuka kula samaki wabichi mara kwa mara au nyama mbichi au iliyopikwa lakini haikuiva vizuri. Utajiepusha na uwezekano wa kula bakteria na vijidudu vingine hatari kwa afya ya mtoto tumboni. Mjamzito anapokula nyama, anatakiwa kuhakikisha imeiva sawasawa.

2. ‘Soseji” na “Sandwich”

Mjamzito haruhusiwi kula ‘soseji’, ‘sandwichi’ za nyama na vyakula vingine vilivyotengenezwa kwa nyama. Inaaminika kuwa nyama zinazoandaliwa kwa ajili ya kutengenezea vyakula kama hivyo, huwa vimewekewa vihifadhi vyakula (preservatives) ambavyo vinaweza visiwe vizuri kwa afya ya mtoto.

3. Samaki wenye zebaki (Mercury)

Wajawazito wamekatazwa kula samaki wenye kiasi kingi cha madini ya zebaki. Ulaji wa zebaji kwa wajawazito umehusishwa na uzaaji wa watoto taahira. Mfano wa samaki hao ni pamoja na Papa, Chuchunge na dagaa wakubwa.

4. Mayai Mabichi

Ulaji wa mayai mabichi au vyakula vilivyochanganywa na mayai mabichi, mjamzito haruhusiwi kuvila. Kuna baadhi ya ‘Ice Cream’ na ‘mayonaizi’ hutengenezwa kwa kuchanganywa na mayai mabichi. Mjamzito amekatazwa kuvila vyakula hivyo.

5. Maini

Epuka ulaji wa maini kwa kiwango kikubwa sana wakati wa ujauzito, Mbali na Maini kuwa na kiwango kikubwa cha madini aina ya chuma ambayo ni muhimu sana kwenye utengenezaji wa damu na kuongeza wingi wa damu kwa mjamzito. Hata hivyo, yana kiasi kikubwa cha Vitamin A ambacho huweza kuwa na madhara kwa mtoto kikizidi.

6. Maziwa mabichi

Maziwa mabichi huweza kuwa na bakteria ajulikanae kama ‘Listeria’, ambaye huweza kusababisha kuharibika kwa mimba. Unapokunywa maziwa, hakikisha yamechemshwa au kama ni ya paketi hakikisha ni yale yaliyoandikwa‘Pasteurized’ na siyo ‘Unpasteurized’.

7. Kafeini (Caffeine)

Ingawa baadhi ya utafiti unaonesha kuwa unywaji wa kiasi kidogo cha kafeini hauna madhara, lakini kuna utafiti mwingine unaonesha kuwa unywaji wa kafeini una uhusiano na kuharibika kwa mimba. Kafeini ni aina ya kirutubisho kinachopatikana ndani ya kahawa.

Iwapo mjamzito atakunywa kahawa, basi anywe kiasi kidogo sana kisichozidi kikombe kimoja kwa siku. Kwa kawaida kahawa hukausha maji mwilini, hivyo unywaji wake husaidia kukauka maji mwilini ambayo ni muhimu sana kwa mjamzito.

Utafiti mwingine unaonesha kuwa kafeini inahusishwa pia na uharibikaji wa mimba, uzaaji wa watoto ‘njiti’ na watoto wenye uzito mdogo. Ni vizuri kunywa maji ya kutosha, maziwa na juisi na kuepuka kunywa vinywaji vyenye kahawa.

8. Pombe

Hakuna ushahidi unaothibitisha kuwa unywaji wa pombe kiasi kidogo wakati wa ujauzito hauna madhara, kwa maana hiyo matumizi ya pombe hayaruhusiwi kabisa wakati wa ujauzito, hata kama ni kidogo.
Unywaji wa pombe wakati wa ujauzito huweza kuathiri ukuaji mzuri wa mtoto. Kutegemeana na kiasi atakachokunywa mjamzito, pombe inaweza kumsababishia mtoto ugonjwa hatari utokanao na pombe (Fetal Alcohol Syndrome).

VYAKULA GANI NI MUHIMU SANA KUTUMIWA NA WAJAWAZITO?

Lishe bora wakati wa ujauzito ni muhimu sana, kwani lishe hii hutumika kwa mama na mtoto anaendelea kukua tumboni. kwa kawaida mahitaji ya chakula na virutubisho mwilini mwa mwanamke huongezeka wakati wa ujauzito na kadri ujauzito unavyoendelea kukua, virutubisho hivyo hutumika kujenga mwili wa mama na mtoto. hivyo maamuzi ya lishe au lishe mama anayopata huathiri pia maendeleo ya mtoto anayekua mwilini mwake. tutaona vyakula muhimu vya kuzingatia lishe bora wakati wa ujauzito na baadhi ya vitu vya kukwepa.

Mlo kamili (balanced diet), ni muhimu kwa ajili ya maendeleo mazuri ya afya ya mjamzito na mtoto tumboni. Pamoja na mlo kamili mjamzito hupewa virutubisho ziada (supplements) kwa ajili ya kuongeza madini kama ya chuma na Foliki. Mlo kamili unajumuisha vyakula vya wanga, protini, mafuta, vitamini, madini na maji kama inavyochambuliwa hapa chini:

- Nafaka na vyakula vya wanga

Vyakula hivi huupa mwili nguvu za kufanya kazi ikiwemo ukuaji wa mtoto tumboni. Vyanzo vya wanga ni kama nafaka mbalimbali(mahindi,mtama,ulezi n.k), viazi, ndizi, mihogo. Ni vizuri mjamzito awe anapata nafaka kamili(whole grains) kama mahindi, ngano na mchele usiokobolewa; cereals n.k.

- Nyama, samaki na vyakula vya protini

Hivi ni muhimu kwenye kuujenga mwili, hasa kipindi cha miwezi wa 4 mpaka wa 9 ambacho viungo mbalimbali vya mtoto vinajengwa. Ni muhimu mama apate vyakula vya protini vya kutosha ili kuhakikisha ukuaji wa mtoto unaenda vizuri. Nyama za kuku, ng’ombe, mbuzi, senene, panzi na wanyama wengine ; vyanzo vya protini za mimea kama maharage, soya, njugu, njegere, karanga,korosho n.k . Samaki, maziwa, mayai ni vyanzo vingine vya protini muhimu

- Vyakula vya mafuta

Hutumika kwenye kuupatia mwili nguvu pamoja na ujengaji wa seli za mwili. Mara nyingi vyakula kama nyama, karanga, ufuta, alizeti,senene, panzi, samaki na matunnda kama maparachichi huwa na mafuta. Ni vizuri kutumia mafuta yatokanayo na mimea ili kupunguza mafuta yenye lehemu(cholesterol) nyingi.

- Mboga za majani na matunda

Matunda na mboga za majani ni sehemu muhimu sana ya mlo wakati wa ujauzito, kwani huupatia mwili vitamini, madini na kambakamba kwa ajili ya kulainisha chakula. Vitamini husaidia kuimarisha kinga ya mwili sambamba na ufanyaji kazi wa mwili. Madini kama ya chuma, kalsiamu, zinki, madini joto(Iodine) na magneziamu ni muhimu kwa ukuaji salama wa mtoto tumboni mwa mama.Vitamini B9 (Foliki asidi) na madini ya chuma hutolewa kama virutubisho ziada kliniki wakati wa ujauzito ili kutosheleza mahitaji ya mwili na kuzuia hatari ya upungufu wa damu kutokea.

- Maji

Maji ni muhimu kwenye mmenyenyo na unyonywaji wa chakula, pia husaidia kuzuia choo kigumu, mwili kuvimba na maambukizi ya mfumo wa mkojo (UTI). Inashauriwa mjamzito anywe maji si chini ya lita 2.3 kwa siku, yanaweza kuwa katika chai, juisi, soda, au maji yenyewe. Ni vema zaidi kama akinywa maji kama maji zaidi na kupunguza vinywaji kama soda.

MFANO WA MPANGILIO WA MLO

Ili kuhakikisha mlo kamili mjamzito anaweza kufuata mfano wa mpangilio wa mlo ufuatao. Katika mpangilio huu inashauriwa kuchagua aina moja ya chakula kutoka katika kila herufi A mpaka E ili kuweza kuupata mlo kamili.

Mfano:

MLO WA ASUBUHI:

A – Chungwa/ Embe/ Ndizi mbivu/ Parachichi
B – Mkate/ Maandazi/ Chapati/ Vitumbua/ Uji
C – Karoti
D – Mayai
E – Maziwa/ Mtindi/ Siagi/ Maziwa ya Soya

MLO WA MCHANA:

A – Parachichi/ Papai/ Ndizi/ Embe na chungwa
B – Ugali/ Wali/ Ndizi/ Makande/ Tambi
C – Mchicha/ matembele/ Mnavu/ Kisamvu/ Spinach/ Kabeji
D – Maharage/ Samaki/ Kuku/ Njugu/ Nyama/ Dagaa
E – Maziwa/ Mtindi/ Siagi/ Maziwa ya Soya.

MLO WA USIKU:

A – Parachichi/ Papai/ Ndizi/ Embe na Chungwa
B – Wali/ Ndizi/ Viazi/ Tambi/ Chapati
C – Mchicha/ Matembele/ Mnavu/ Kisamvu/ Spinach/ Kabeji,
D – Maharage/ Samaki/ Kuku/ Njugu/ Nyama/ Dagaa
E – Maziwa/Mtindi/Siagi/Maziwa ya Soya.

SOMA Zaidi Hapa: Kuhusu Vyakula vya kuepuka Wakati wa Ujauzito

Cr Source:

  • Afyatrack
  • Healthline
  • WebMd

KWA USHAURI ZAIDI,ELIMU AU TIBA JUU YA TATIZO LOLOTE TUWASILIANE KWA NAMBA +255758286584.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!