WHO imetangaza kuidhinishwa kwa chanjo ya MVA-BN kama chanjo ya kwanza ya ugonjwa wa mpox

WHO imetangaza kuidhinishwa kwa chanjo ya MVA-BN kama chanjo ya kwanza ya ugonjwa wa mpox

Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limetangaza kuidhinishwa kwa chanjo ya MVA-BN kama chanjo ya kwanza dhidi ya ugonjwa wa mpox. Hatua hii inatarajiwa kurahisisha upatikanaji wa haraka wa chanjo hiyo, hususani katika maeneo yaliyoathirika zaidi, ili kupunguza maambukizi na kudhibiti mlipuko wa ugonjwa huo hatari. 

Chanjo hii imeidhinishwa kufuatia tathmini ya shirika la udhibiti la Ulaya pamoja na taarifa zilizotolewa na mtengenezaji, Bavarian Nordic A/S.

"Kupitishwa kwa chanjo hii ni hatua muhimu katika mapambano yetu dhidi ya mpox, hasa kwa mlipuko wa sasa barani Afrika na kwa siku za usoni. Tunahitaji kuharakisha upatikanaji wa chanjo, michango na usambazaji ili kuhakikisha upatikanaji sawa katika maeneo yenye uhitaji mkubwa, pamoja na matumizi ya zana nyingine za afya ya umma ili kuzuia maambukizi, kukomesha usambazaji na kuokoa maisha." Amesema Mkurugenzi mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus.

Chanjo ya MVA-BN inapaswa kutolewa kwa watu wenye umri wa zaidi ya miaka 18 kama sindano mbili zenye wiki nne kati ya dozi. Chanjo hiyo inaweza kuhifadhiwa kwa hadi wiki nane katika joto la nyuzi 2-8°C baada ya kuhifadhiwa kwenye hali ya baridi kali.

WHO imesisitiza kwamba licha ya chanjo hii kutokuwa na leseni kwa watoto chini ya miaka 18, inaweza kutumika kwa watu wenye umri mdogo katika mazingira ya mlipuko. Aidha, WHO inapendekeza matumizi ya dozi moja ya chanjo wakati wa uhaba wa chanjo.

Ripoti zinaonesha kwamba dozi moja ya chanjo ya MVA-BN inatoa kinga ya asilimia 76 dhidi ya mpox, huku dozi mbili zikifikia asilimia 82. Usalama wa chanjo hii umethibitishwa katika tafiti za kliniki na matumizi ya ulimwenguni kote tangu mlipuko wa mwaka 2022.

Hivi sasa, WHO inashirikiana na mashirika mengine kuharakisha upatikanaji wa chanjo nyingine mbili dhidi ya mpox, LC-16 na ACAM2000 huku mlango wa dharura kwa bidhaa za uchunguzi wa mpox pia umefunguliwa, WHO ikipokea maombi sita ya matumizi ya dharura.

Mpox imeendelea kuwa tishio kubwa, hususani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambapo mlipuko umeongezeka, na WHO ilitangaza hali hiyo kuwa dharura ya afya ya umma ya kimataifa mnamo Agosti 14, 2024 huku tangu kuanza kwa mlipuko wa kimataifa mwaka 2022, zaidi ya nchi 120 zimethibitisha kesi 103,000 za mpox, huku vifo 723 vikirekodiwa mwaka 2024 pekee.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!