Fahamu kuhusu Ubongo wa Nzi unavyoonekana

Fahamu kuhusu Ubongo wa Nzi unavyoonekana

Wanaweza kutembea, kuelea juu na madume wanaweza hata kuimba nyimbo za mapenzi ili kuwavutia majike - yote haya kwa ubongo mdogo kuliko kichwa cha pini.

Wanasayansi wanaotafiti ubongo wa nzi wamegundua ulipo, umbo na muingiliano wa kila seli moja kati ya seli zake 130,000 na viunganishi vyake milioni 50.

Ni uchambuzi wa kina wa ubongo wa mdudu.

Mtaalamu mmoja mashuhuri wa ubongo asiyehusika na utafiti huo mpya ameeleza kuwa haya ni mafanikio makubwa katika kuzielewa bongo zetu wenyewe.



Dk Gregory Jefferis, wa Maabara ya Utafiti wa Kimatibabu (LMB), katika chuo Kikuu cha Cambridge, aliambia BBC, kwa sasa hatujui jinsi mtandao wa seli za ubongo katika vichwa vyetu zinavyoingiliana na kila moja.

"Kuna mungiliano gani? Ni kwa namna gani mawimbi hutiririka kupitia mfumo unaoweza kuturuhusu kuchakata taarifa ili kutambua uso wa mtu, au kusikia sauti na kugeuza maneno na kuwa mawimbi ya umeme?



"Uchoraji wa ramani ya ubongo wa inzi ni wa kuvutia sana na utatusaidia kuelewa jinsi akili zetu wenyewe zinavyofanya kazi."

Tuna chembechembe za nyuroni kwenye ubongo milioni kwa milioni, zaidi ya zile za nzi aliyefanyiwa utafiti. Kwa hivyo mchoro wa ubongo wa wadudu unawezaje kuwasaidia wanasayansi kujifunza zaidi.

Picha ambazo wanasayansi wametoa, ambazo zilichapishwa katika jarida la Nature, zinaonyesha nyuzi nyuzi mithili ya wavu.

Muundo wake ndio unaoshikilia ufunguo wa kuelewa jinsi kiungo hicho kidogo kinavyoweza kutekeleza kazi nyingi zenye kubwa na za kimahesabu. Kutengeneza kompyuta ya ukubwa wa mbegu ya nafaka yenye uwezo wa kazi kama ubongo wa nzi ni uwezo ambao sayansi ya sasa haijafikia.

Dk Mala Murthy, mhusika mwingine katika mradi huo, kutoka Chuo Kikuu cha Princeton, anasema picha hizo mpya zitaleta mabadiliko kwa wanasayansi wa neva.

"Itasaidia watafiti wanaojaribu kuelewa jinsi ubongo wenye afya unavyofanya kazi. Katika siku zijazo tunatumai itawezekana kuelewa kile kinachotokea katika akili zetu.

Hayo ni maoni yanayoungwa mkono na Dk Lucia Prieto Godino, kiongozi wa timu ya utafiti wa ubongo katika Taasisi ya Francis Crick huko London, ambaye hayuko katika timu ya watafiti wa ubongo wa nzi.

"Watafiti wamefanikiwa kugundua mfumo wa seli wa mnyoo mwenye nyuzi nyuzi 300 na funza ambaye ana elfu tatu, lakini kuelewa muunganiko wa seli za mdudu mwenye nyuzi nyuzi 130,000 ni kazi ya kiufundi ya kushangaza ambayo inafungua njia ya kupata kuuelewa ubongo mkubwa kama vile wa panya na labda katika miongo kadhaa ubongo wetu wenyewe."

Ulivyofanyika Utafiti huo ulifanywa kwa kukata vipande vipande ubongo wa inzi na kuvipiga picha kila moja - vipande 7,000. Kisha timu ya Princeton ikatumia akili bandia kutoa maumbo na miunganisho ya niuroni zote. Lakini akili bandia haikukamilisha kazi hiyo - na watafiti walilazimika kurekebisha makosa zaidi ya milioni tatu kwa mkono.

Hii yenyewe ilikuwa safari ya kiufundi, lakini kazi ilikuwa nusu tu. Ramani yenyewe haikuwa na maana isipokuwa kuwe na maelezo ya kazi ya kila nyuzi ya ubongo huo, anasema Dk Philipp Schlegel, ambaye pia anatoka katika Maabara ya Utafiti wa Kimatibabu.

"Kuelezea nyuroni ni kama kuweka majina ya mitaa na miji, saa za kufungua biashara, nambari za simu, maoni, n.k. kwenye ramani ya google."



Dk Schlegel anaamini ulimwengu wa sayansi ya neva utaona "mfululizo wa uvumbuzi katika miaka michache ijayo" kutokana na ramani hii mpya.

Ubongo wa mwanadamu ni mkubwa zaidi kuliko wa inzi, na bado hatuna teknolojia ya kunasa taarifa zote kuhusu nyaya zake.

Lakini watafiti wanaamini katika miaka 30 itawezekana kuuelewa ubongo wa binaadamu wote. Ubongo wa nzi, wanasema, ni mwanzo wa ufahamu mpya, wa kina wa jinsi akili zetu wenyewe zinavyofanya kazi.

Utafiti huo umefanywa kwa ushirikiano mkubwa wa wanasayansi wa kimataifa, na umepewa jina la FlyWire Consortium.

Chanzo: BBC

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!