Ticker

6/recent/ticker-posts

Maambukizi Ya Malaria Yapungua Hadi Asilimia 8.1 Kwa Mwaka 2015-2022



Maambukizi Ya Malaria Yapungua Hadi Asilimia 8.1 Kwa Mwaka 2015-2022

Wizara ya afya kupitia mpango wa taifa wa kudhibiti malaria kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI imepunguza kiwango cha malaria kwa asilimia 45 kutoka 14.8 ya mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 8.1 mwaka 2022.

Hayo yamebainishwa na Naibu waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge na Masuala ya Ukimwi kilichofanyika katika ukumbi wa bunge Jijini Dodoma.

Dkt. Mollel amesema kuwa, Serikali imetekeleza mikakati ya udhibiti wa mbu waenezao Malaria kwa njia ya utengamano pamoja na ugunduzi, matibabu na tiba kinga dhidi ya malaria ambapo imewezesha mafanikio hayo kwa takribani miaka 8 na kupunguza wagonjwa wa malaria wanaotibiwa kama wagonjwa wa nje (OPD) kwa asilimia 55.

“Serikali imetekeleza afua mbali mbali kwa takriban miaka minane na kufanikiwa kupunguza kiwango cha malaria kwa asilimia 45 kutoka 14.8 hadi 8.1 pamoja na kupunguza wagonjwa wa nje kwa asilimia 55 ambapo awali walikua ni milioni 7.7 hadi 3.5 kwa mwaka 2023”. Amesema Dkt. Mollel

Aidha, Dkt. Mollel amesema kuwa kwa sasa mpango wa taifa wa kudhibiti malaria unatekeleza mpango mkakati wa sita wa mwaka 2021 mpaka 2025 wenye lengo la kupunguza kiwango cha chini kutoka asilimia 7.5 (2017) hadi 3.5 ifikapo 2025

Kwa Upande wake Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Bi Bernadeta Mushashu ameishauri serikali kuongeza afua za kutokomeza malaria katika mikoa iliyo katika hatari  ya maambukiza ya malaria kama vile Tabora unaoongoza  kwa asilimia 23.4, Mtwara kwa asilimia 20, Kagera asilimia 18, Shinyanga 16%na Mara 15%.

Aidha ameipongeza Serikali kwa juhudi na malengo ya kuendelea kutekeleza afua za kutokomeza malaria pamoja na kufanikiwa kupunguza mpaka chini ya asilimia katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Dodoma, Singida, Iringa, Songwe, Dar es Salaam na Mwanza.

Hata hivyo wametoa rai kwa wananchi kuendelea kutekeleza ushauri wa madaktari kuhusu matumizi sahihi ya vyandarua pamoja na kuweka mazingira yanayotuzunguka safi na salama  ili kuzuia mazalia ya viluilui ya mbu.