Mafuriko Sudan Kusini yasababisha Zaidi ya watu 241,000 kutoroka makazi yao
Watu 893,000 wameathiriwa na mafuriko nchini Sudani Kusini na zaidi ya watu 241,000 wameyakimbia makazi yao, kulingana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Kibinadamu (OCHA).
"Mafuriko yanaendelea kuathiri na kuwahamisha watu kote nchini," OCHA aimesema. "Mvua kubwa na mafuriko yamefanya barabara kuu 15 kutopitika, na kuzuia ufikiaji" kwa wakaazi.
Kulingana na OCHA, takriban watu 893,000 wameathiriwa na mafuriko katika kaunti 42 na katika eneo la kiutawala la Abyei, eneo linalozozaniwa na Sudani na Sudani Kusini. Zaidi ya 40% ya walioathiriwa wanaishi katika majimbo ya Unity na Warrap kaskazini.
Zaidi ya watu 241,000 waliokimbia makazi yao "ili kupata makazi juu kwenye milima" wanatoka kaunti 16 na eneo la Abyei, OCHA imesema. Sudani Kusini inakabiliwa na mafuriko mabaya zaidi kuwahi kutokea katika miongo kadhaa, kulingana na mashirika ya kibinadamu.
Benki ya Dunia ilibaini mnamo Oktoba 1 kwamba mafuriko yanazidisha "hali ambayo tayari ni mbaya ya kibinadamu, inayokumbwa na uhaba mkubwa wa chakula, kuzorota kwa uchumi, migogoro inayoendelea, magonjwa ya milipuko, na athari za mzozo nchini Sudani."
Vita vya Sudani vimesababisha zaidi ya watu 797,000 kuondoka Sudani Kusini, asilimia 80 kati yao wakiwa ni raia wa Sudani Kusini.
Makubaliano ya amani mwaka 2018 yalimaliza miaka mitano ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudani Kusini, lakini nchi hiyo, iliyojitawala tangu mwaka 2011, inakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu na ukosefu wa rasilimali. Serikali imepoteza chanzo chake kikuu cha mapato baada ya bomba la mafuta kuharibiwa na mapigano katika nchi jirani ya Sudani.