Magonjwa ya Moyo huua ZAIDI ya wagonjwa milioni 20 kila mwaka duniani kote
Magonjwa ya Moyo huua ZAIDI ya wagonjwa milioni 20 kila mwaka duniani kote
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo Tanzania na Rais wa Chama cha madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo, Robert Mvungi.
ZAIDI ya wagonjwa milioni 20 wanafariki kila mwaka duniani kote kwasababu ya magonjwa ya moyo ambayo kwa asilimia 80 yanatokea kwenye nchi za uchumi wa kati na chini.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam na Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo Tanzania na Rais wa Chama cha madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo, Robert Mvungi, wakati wakisherehekea siku ya moyo Duniani ambayo ufanyika kila Septemba 29 ya kila mwaka na kwa mwaka huu iliandaliwa na Hospitali ya Aga Khan kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo Tanzania. Washiriki walipata punguzo la asilimia 50 kwenye chunguzi za ziada.
Dk. Mvungi alisema takribani makundi yote yanaathirika na matatizo ya moyo kutokana na uzito uliozidi kiwango cha kawaida, shinikizo la damu, kisukari, damu kuwa juu, kuvuta sigara na kutofanya mazoezi.
“Chukua hatua kabla haujapata matatizo ya moyo kwasababu haya matatizo yanachukua rasilimali kubwa kuyatibu kwahiyo watu wanasema kinga ni bora kuliko tiba tujitahidi kufanya mazoezi na kuzingatia lishe bora”
Aidha, alisema chama chao cha madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo Tanzania watafungua kampeni ambayo haitaishia mjini pekee itafika vijijini na sehemu zote za nchi ili kutoa elimu kuhusu magonjwa hayo na kuchukua hatua.
“Tunajua serikali yetu inajitahidi kuweka mikakati mbalimbali kuhusu magonjwa ya moyo, lakini bado haijawafikia walengwa wote hapa Tanzania, tunataka tuwafikie walengwa hata vijijini hivyo kupitia siku hii mkakati ni kwamba tuweze kutoa elimu kuwafikia watu waweze kujua matatizo ya moyo, wajikinge na wachukue hatua” alisema.
Akizungumza kwa niaba ya Daktari Bingwa wa Moyo kutoka Hospitali ya Aga Khan, Dk. Julius Msukuya, alisema kati ya asilimia 25 hadi 30 ya wagonjwa ambao wanawapokea katika hospitali ya Aga Khan wanamagonjwa ya moyo yakiwa ni magonjwa mtambuko.
Alisema wagonjwa ambao wanawaona ni zaidi ya asilimia 30 hadi 50 wana shida ya moyo na matibabu yake yameimarika kwa kuzingatia chakula, mazoezi na usaidizi wa dawa kutoka kwa madktari.
“Usipuuzie dalili za magonjwa ya moyo, fanya uamuzi wa haraka dhidi ya ugonjwa wa shambulizi la moyo, katika siku hii ya moyo duniani ni muhimu tuweke afya ya moyo kuwa kipaumbele kwa kujifunza kutambua dalili za awali za shambulio la moyo, hatua za haraka zinaweza kufanya tofauti kubwa katika matokeo ya matibabu na tunaweza kuongeza uelewa na kukuza jamii yenye afya bora ya moyo”
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!