Ticker

6/recent/ticker-posts

Nini hutokea kwenye Ubongo Mtu anapokaribia kufa?



Nini hutokea kwenye Ubongo Mtu anapokaribia kufa?

Mwaka 2023, watafiti walichapisha utafiti uliochunguza wagonjwa wanne ambao walikuwa katika usingizi mzito (coma) wakiwa katika mashine.

"Walikuwa wakifa kutokana na magonjwa mbalimbali," anasema mwanasayansi wa mishipa ya fahamu (neva), na Profesa wa Chuo Kikuu cha Michigan, Jimo Borjigin.

Madaktari na familia walipofikia makubaliano kwamba hawakuwa na jambo lolote la matibabu ambalo wangeweza kufanya, waliamua kuziondoa mashine. Kwa ruhusa kutoka jamaa zao, mitambo ya upumuaji iliondolewa.

Watafiti waligundua katika wagonjwa wawili, shughuli za ubongo zinazohusishwa na kazi za utambuzi zilionekana. Mawimbi ya gamma, katika ubongo yaligunduliwa, ambayo yanahusika katika uchakataji wa taarifa na kumbukumbu.

Kwa wanadamu, ni sehemu fulani tu za ubongo zinazoamshwa unapokaribia kufa. Haya ni maeneo yanayohusiana na kazi za fahamu za ubongo.

Mojawapo ni sehemu ya nyuma ya ubongo inayowajibika kwa utambuzi wa hisia, pia ndoto na maono ya kuona.

Eneo jingine ambalo waliona limeamshwa ni eneo linaloitwa Wernicke, linalohusishwa na lugha, kuzungumza na kusikiliza. Liko karibu na masikio yetu, sehemu hiyo ni muhimu sana si tu kwa kuhifadhi kumbukumbu, lakini kwa kazi nyingine za utambuzi.

Profesa anasema eneo la upande wa kulia la ubongo huhusika na hisia za huruma.

"Wagonjwa wengi ambao wamenusurika kifo kutokana na mshituko wa moyo ama walikaribia kufa, wanasema walipata hisia kubwa za huruma."

Karibu na kifo

Katika historia, watu wengi ambao wamekaribia kufa wamezungumza juu ya kuweza kukumbuka nyakati muhimu za maisha yao; wengi wameona mwanga mkali; wengine hujihisi wameiacha miili yao, wakiinuka na kuona kile kilichokuwa kikiendelea karibu nao.

Utafiti wa 2023 unabainisha kuwa katika kundi la watu waliopata mshtuko wa moyo, 20% au 25% waliripoti kuona mwanga, ikimaanisha ubongo uliamsha eneo la kuona.

"Baadhi ya wagonjwa walionusurika kifo wameripoti kusikia kilichokuwa kikiendelea wakati wa upasuaji wao au kile ambacho wahudumu wa afya waliowaokoa walichokuwa wakikisema."

Inawezekanaje mtu anaweza kuona mwanga, kusikia sauti, kuhisi mwili umeondoka na kuelea hewani? "Hayo yote ni sehemu ya kazi ya ubongo," anasema Profesa.

"Kwa sababu wataalamu wa matibabu wanafikiri ubongo haufanyi kazi wakati mtu anapokaribia kufa, kuna wale wanaoamini shughuli hizi zote hutokea nje ya mwili, yaani ni kitu kisicho cha kawaida."

"2013 tulipochapisha utafiti wa kwanza wa wanyama, tuliandika, wazo kwamba hali hiyo hutokea nje ya mwili haliwezi kuthibitishwa."

''Tangu awali, naamini matukio hayo hutokea kwenye ubongo, ingawa ni matukio ya kushangaza kwa sababu inadhaniwa kuwa ubongo haufanyi kazi wakati unapopata mshtuko wa moyo."

"Ninaamini kwamba matukio ya karibu kufa huja kutokana na shughuli za ubongo ambazo hutokea kabla ya ubongo kukoma kufanya kazi kabisa," anasema Borjigin.

Uelewa wa zamani

Borjigin anakubali kwamba utafiti wake kwa wanadamu ni mdogo sana na utafiti zaidi unahitajika juu ya kile kinachotokea katika ubongo tunapokufa.

"Ubongo, badala ya kuwa na shughuli kidogo, huwa na shughuli nyingi wakati wa mshtuko wa moyo. Tunahitaji kuboresha uelewa wetu kuhusu kazi ya ubongo wakati wa shida kama hiyo."

Anafikiri ongezeko la shughuli za ubongo ni sehemu ya mbinu ya ubongo kuishi wakati unapokosa oksijeni .

"Wanyama, panya na wanadamu, wana utaratibu wa asili wa kukabiliana na ukosefu wa oksijeni."

"Uelewa wetu wa sasa ni kwamba, moyo unaposimama, ubongo hufa tu, tunaamini ubongo hauwezi kukabiliana na kusimama kwa moyo."

Lakini anasema – hatujui ikiwa hilo ni kweli.