Ticker

6/recent/ticker-posts

Wagonjwa zaidi ya 23,000 wamepatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa mkoa wa Njombe



Wagonjwa zaidi ya 23,000 wamepatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa mkoa wa Njombe 

Wagonjwa zaidi ya 23,000 wamepatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa mkoa wa Njombe huku wagonjwa wa dharura na mahututi wakiwa 1,322 katika kipindi cha mwezi Januari hadi Septemba mwaka huu.

Hayo yameelezwa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani mkoa wa Njombe Dk. Gilbert Kwesi katika uzinduzi wa huduma ya uchunguzi wa magonjwa ya mfumo wa chakula (ENDOSCOPY UNIT) uliofanyika katika hospitali hiyo.

Dk. Kwesi amesema magonjwa hayo ya mfumo wa chakula mchanganyiko yamekuwa yakiongoza kwa kuwa na idadi ya wagonjwa wengi ambapo kwa kipindi cha Januari hadi Septemba wagonjwa 566 wamefanyiwa uchunguzi na kutibiwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Njombe Anthony Mtaka mara baada ya kuzindua huduma hiyo amewataka watumishi wa hospitali kuendelea kutoa huduma bora sambamba na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.

“Fanyeni kazi kwa kuzingatia maadili lakini tembeeni kifua mbele kwa sababu serikali inaendelea kuhakikisha mnafanya kazi katika mazingira rafiki na kuridhisha pamoja na kutatua matatizo yenu ya kimaslahi,” amesema Mtaka.

Katibu Tawala Mkoa wa Njombe,Judica Omary ametoa rai kwa watoa huduma hao kuongeza ufanisi ili maboresho ya vifaa tiba yaweze kuleta tija.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Kissa Kasongwa ametoa wito kwa wakazi wa Njombe kuiamini hospitali ya rufaa ya mkoa huo kutokana na uwapo wa vifaa tiba vya kibingwa vya teknolojia ya kisasa na huduma zake zikiwa ni bora.

Kuzinduliwa kwa huduma ya tiba kwa wenye matatizo katika mfumo wa chakula kunaifanya hospitali ya rufaa Mkoa wa Njombe kuwa na huduma zote muhimu ambazo awali wakazi wa mkoa huo walilazimika kuzifuata katika hospitali ya Taifa Muhimbili.