Ticker

6/recent/ticker-posts

Wapandikizwa Ini baada ya kula Uyoga wenye sumu



Wapandikizwa Ini baada ya kula Uyoga wenye sumu

Mwanamume mmoja nchini Ujerumani na watoto wawili wamelazimika kupandikizwa ini katika Hospitali ya Chuo Kikuu katika mji wa magharibi mwa Ujerumani wa Essen, baada ya kula uyoga wenye sumu.

Mgonjwa wa nne, ambaye ni mvulana mdogo wa miaka mitano, alipata nafuu bila kupandikizwa ini, imesema hospitali hiyo. Wote wanne, mmoja wao akiwa ni baba wa mmoja wa watoto hao, wamekuwa katika uangalizi wa wagonjwa mahututi katika hospitali hiyo tangu siku ya Jumanne.

"Hali za wagonjwa wote zinaendelea vizuri na wanafuatiliwa kwa karibu na kwa umakini," ilisema taarifa iliyotolewa na hospitali hiyo.

Wagonjwa hao walilazwa hospitalini wakiwa na hali mbaya. Wawili walifanyiwa upasuaji wa kupandikiza ini muda mfupi baada ya kufikishwa hospitali na mtoto mmoja alifanyiwa baadaye.

Uyoga huo aina ya Amanita huliwa, lakini pia una vimelea vya sumu.

Katika kisa tofauti huko mjini Münster, mgonjwa mmoja mwanamke ameendelea kupatiwa matibabu ya kina baada ya kula uyoga wenye sumu wiki iliyopita. Inaaminika kuwa mgonjwa huyo alikula uyoga wa aina hiyo ya Amanita.

Msemaji katika hospitali anakotibiwa mgonjwa huyo alisema siku ya Jumatatu kwamba mgonjwa huyo bado ana hali mbaya na anapatiwa huduma ya wagonjwa mahututi. Aidha pia bado wanatafuta mtu anayeweza kuchangia ini ili waweze kumfanyia upandikizaji.

Bado haijafahamika ikiwa wagonjwa hao walichuma uyoga mwituni au walikula ni wapi walipoula uyoga huo.