Ticker

6/recent/ticker-posts

Watu milioni 730 wanakabiliwa na njaa duniani kote-FAO



Huu ni Ujumbe wa FAO kwa dunia, Siku ya chakula duniani

Jana ilikuwa ni siku ya chakula duniani,Tarehe 16 October, ambako huko Roma, Italia makao makuu ya shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO, kumefanyika tukio maalum la kuadhimisha siku hiyo, washiriki wakisisitiza umuhimu wa kila mtu duniani kupata chakula bora, cha kutosha, salama na kwa bei nafuu.

Watu wana uwezekano mkubwa wa kukabiliwa na uhaba wa chakula na utapiamlo ikiwa hawawezi kumudu lishe bora.

Maadhimisho yamefanyika wakati kukiwa na mivutano na mizozo duniani, sambamba na madhara ya mabadiliko ya tabianchi, mambo ambayo yanachochea mamilioni ya watu duniani kote kukumbwa na njaa huku mabilioni wengine wakiwa hawana uwezo wa kupata lishe bora.

Ujumbe wa Mkurugenzi Mkuu wa FAO

Akifungua maadhimisho hayo, Mkurugenzi mkuu wa FAO, QU Dongyu amesema maudhui ya siku hii mwaka huu ambayo ni Haki ya Chakula Kwa Maisha Bora na Mustakabali Bora, yamekuja wakati muhimu kukumbusha kwamba watu wote wana haki ya kupata chakula cha kutosha.

“Natoa wito kwa ahadi mpya ya kujenga mifumo ya kilimo cha mazao ya chakula iliyo fanisi, jumuishi, yenye mnepo na endelevu zaidi itakayowezesha kulisha vema dunia.”

Qyu amesema mifumo ya aina hiyo inatakiwa kusaidia wakulima wadogo, wakulima wa kaya na wafanyabiashara wadogo kwenye mnyororo wa thamani ambao katika nchi nyingi ndio msingi wa kuwezesha kuzalisha vyakula tofauti tofauti vyenye lishe na kuwezesha vipatikane na viwafikie watu, na wakati huo huo wakihifadhi tamaduni za asili za vyakula.

Watu milioni 730 wakikabiliwa na njaa duniani kote na wengine zaidi ya bilioni 2.8 wanashindwa kupata lishe bora, “hatuna wakati wa kupoteza, na lazima tuchukue hatua,” amesema Mkurugenzi Mkuu huyo wa FAO