Kusitishwa kwa ufadhili wa Marekani na Athari kwa Ugonjwa wa Ukimwi;UNAIDS

Kusitishwa kwa ufadhili wa Marekani na Athari kwa Ugonjwa wa Ukimwi;UNAIDS

#1

Kusitishwa kwa ufadhili wa Marekani na Athari kwa Ugonjwa wa Ukimwi;UNAIDS



Shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na ukimwi UNAIDS leo limeonya kwamba kusitishwa kwa ufadhili wa Marekani sio tu janga kwa vita dhidi ya gonjwa hilo bali ni chachu ya vifo na ongezeko la maambukizi mapya. Flora Nducha amefuatilia onyo hilo lililotolewa leo mjini Geneva Uswisi na Mkurugenzi mtendaji wa UNAUDS Winnie Byanyima alipozungumza na waandishi wa habari.

Bi. Byanyima amewaambia waandishi wa habari kwamba serikali ya Marekani imekuwa mfadhili mkubwa wa mipango ya kukabiliana na UKIMWI, hasa kupitia Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR).

Hata hivyo, kukatwa kwa msaada wa kifedha sasa kunahatarisha programu muhimu zinazotoa matibabu ya kuokoa maisha, huduma za kuzuia maambukizi, na utafiti wa kisayansi hasa kwa nchi ambazo msaada huo ni tegemeo kubwa mathalani amesema.

UNAIDS inatahadharisha kuwa bila msaada wa kifedha wa kutosha, mamilioni ya watu, hasa katika nchi zenye kipato cha chini, wanaweza kukosa huduma muhimu za UKIMWI na hasa wale wanaotegemea dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo ili kuendelea kuishi akisema “Hata kufurugwa kwa muda mfupi kwa matibabu kuna athari kubwa kwa watu wanaoishi na HIV. Endapo mtu ataruka kunywa dozi kutamsababishia usugu wa dawa , hii itaongeza idadi ya virusi, na hii itaongeza maambukizi.”



 Bi Winnie amesema waathirika wakubwa katika zahma hii ya ukataji ufadhili ni jamii zilizo hatarini, zikiwemo wanawake, watoto, na makundi yaliyotengwa ambayo tayari yanakumbwa na changamoto za kupata huduma za afya hususan  Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambako kiwango cha maambukizi ya UKIMWI bado ni cha juu, na hivyo kupungua kwa msaada wa kifedha kunaweza kufuta mafanikio yaliyopatikana katika kupunguza maambukizi na kuboresha upatikanaji wa matibabu.

Ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kuzuia kurudi nyuma kwa maendeleo katika juhudi za kimataifa za kumaliza janga la UKIMWI ifikapo 2030.

UNAIDS na mashirika mengine ya afya duniani yameitaka serikali ya Marekani kufikiria upya uamuzi wake wa kupunguza ufadhili, yakisisitiza kuwa uwekezaji endelevu ni muhimu ili kuendelea kupiga hatua katika mapambano dhidi ya UKIMWI.

Tathimini ya bara la Afrika

Akizungumzia Afrika ambako Mashariki na Kusini mwa bara hilo kunabeba asilimia 53 ya mzigo wa VVU duniani  Bi. Byanyima ameonya kwamba kufunga ghafla vituo vya msaada kwa wasichana na wanawake vijana kutakuwa na madhara makubwa, kwa sababu zaidi ya asilimia 60 ya maambukizi mapya ya VVU barani humo yanawaathiri wasichana na wanawake vijana.

Akizungumza na UN News mapema mwezi huu, mkuu wa ofisi ya UNAIDS nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Susan Kasedde, alisema bado kuna maswali makubwa kuhusu kiwango na upeo wa kupunguzwa kwa ufadhili wa mpango wa PEPFAR wa Marekani.

Mpango huu, ulioanzishwa mwaka 2003, unalenga kuzuia na kudhibiti maambukizi ya VVU ukiwa ni mpango wa dharura wa urais wa Marekani ambao unakadiriwa kuwa umeokoa maisha ya takriban watu milioni 26.

Kwa sasa, kuna takriban watu 520,000 wanaoishi na VVU nchini DRC, wakiwemo wanawake 300,000 na watoto 50,000. Janga hili linaendelea kukua, kwani idadi ya maambukizi mapya karibu inazidi mara mbili idadi ya vifo vinavyohusiana na ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa UNAIDS Mchango wa PEPFAR uliotarajiwa kwa mwaka wa kifedha wa 2025 ulikuwa ni dola milioni 105, na unalenga kutoa matibabu kwa nusu ya watu wanaoishi na VVU nchini DRCambao ni takriban watu 209,000.

"Hii inamaanisha kuwa kwa sasa tuna watu 440,000 wanaoishi na VVU ambao wanapata matibabu. Kupitia matibabu haya, wanaendelea kuishi," alisema Bi. Kasedde.

Aliongeza kuwa "Na matibabu haya hayawezi kufanikiwa bila uwezo wa kiutendaji. Matibabu hayawezi kutolewa ikiwa hakuna mnyororo wa ugavi unaofanya kazi ipasavyo," alisisitiza, akionyesha kuwa hatua dhidi ya VVU nchini DRC zinategemea kwa kiasi kikubwa programu zinazoingiliana na kusaidiana.




TOA MAONI YAKO HAPA(REPLY BELOW👇)


image quote pre code