Jeneza la Papa Francis kufunikwa kesho Ijumaa
Ibada ya kufunga jeneza la Hayati Papa Francis inatarajiwa kufanyika kesho Ijumaa usiku Aprili 25, 2025, katika Basilika ya Mtakatifu Petro, Vatican.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Jumatano Aprili 23, 2025 na Mshereheshaji wa Nyumba ya Kipapa Jumatano, jeneza hilo litafungwa saa mbili kamili usiku kwa saa za Ulaya, sawa na saa 3:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki na Kati.
Ibada hiyo itaongozwa na Mwadhama Kardinali, Kevin Joseph Farrell, Camerlengo wa Kanisa Takatifu la Roma, kwa mujibu wa kanuni rasmi za mazishi ya Papa wa Roma (Ordo Exsequiarum Romani Pontificis nn. 66-81).
Mshereheshaji wa maadhimisho ya Kipapa, Askofu Mkuu Diego Ravelli, amesema kuwa maandalizi yote yamekamilika na kwamba ibada hiyo ni sehemu ya mfululizo wa taratibu za heshima za mwisho kwa kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani.
Reply
image quote pre code